Monday, June 4, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: MBUNGE WA CCM AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA RUSHWA


MBUNGE wa Jimbo la Bahi (CCM), Omary Ahmed Badwel (43) leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam,na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), kwa makosa ya kupokea rushwa ya shilingi milioni moja kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Jonathan Liana.
Wakili wa Takukuru, Janeth Machullia na Ben Lincoln walidai mbele ya Hakimu Mkazi Faisal Kahamba kuwa mshitakiwa huyo anakabiliwa na makosa mawili ya rushwa. 

 Wakili Machullia alidai kuwa kosa la kwanza ni la rushwa kinyume na kifungu cha 15(1) (a) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11 ya mwaka 2007, kuwa kati ya Mei 30 na Juni 2 mwaka huu katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam , Badwel akiwa ni Mbunge wa Bahi na Mjumbe Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC) na wakati huo akiwa ni ofisa wa serikali kwa maana ya sheria ya Takukuru, alitenda kosa la kushawishi ili apewe rushwa ya jumla ya Shilingi milioni nane toka kwa Liana ili aweze kuwapelekea wajumbe wenzake wa Kamati hiyo ya Bunge ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya mwaka 2011/2012 ya Halmashauri hiyo.
 
 Wakili Machullia alidai kuwa, shitaka la pili ni kwamba kati ya Juni 2 mwaka huu, katika Hoteli ya Peacock, mshitakiwa akiwa na nyadhifa zake zote hizo alipokea rushwa ya milioni moja kutoka kwa Liana ili aweze kwenda kuwashawishi wajumbe wa Kamati hiyo ili waweze kuipitisha ripoti ya fedha ya Halmashauri ya Mkuranga huku akijua kufanya hivyo ni kosa. 

Hata hivyo mshitakiwa huyo anayetetewa na wakili wa kujitegemea Mpare Mpoki alikanusha mashitaka yote na wakili wa Machullia alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

No comments:

Post a Comment