Thursday, June 28, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS:TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UKATILI,UNYAMA NA VITENDO VYA KUTWEZA ALIVYOFANYIWA MTETEZI WA HAKI ZA BINADAMU DKT. ULIMBOKA STEVEN

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kwa kushirikiana na Mtandao Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRD- Coalition) tunalaani kwa nguvu zote kitendo cha shambulio la kinyama na la kutweza alilofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka.

Tunapenda kuujulisha umma wote kwa ujumla kuwa, tumepokea taarifa kuwa, watu wasiojulikana wakiwa na silaha ( ambao wanasadikiwa kuwa ni mawakala wa dola) siku na saa husika, pale karibu na klabu ya Leaders maeneo ya wilaya ya Kinondoni, jijini Dar-es-salaam,walimkamata(kumteka)Dkt Ulimboka.Walimuingiza kwenye gari dogo kwa nguvu. Gari hilo lilikua jeusi lisilo na namba zinazoeleweka. Hatimaye walimchukua kwa nguvu na kumfunga macho kwa kitambaa cheusi usoni na kumfunga kwa kamba miguuni na mikononi huku wakimpiga sana kwa vitu mbali mbali ikiwemo kitako cha bunduki na vitu vingine vyenye ncha kali.Matokeo ya vipigo hivyo vya kinyama vimesababishia daktari huyu kupata majereha na uvimbe katika sehemu nyingi za mwili wake kuanzia utosini hadi miguuni. Kwa kifupi ni kuwa alitekwa nyara na kuteswa.

Alfajiri ya tarehe 27Juni 2012, tulipata taarifa ya mkasa huu na kuwa Dkt. Ulimboka ambaye mwanzoni alikua amepotea alikuwa amepatikana na alikua ameshikiliwa katika kituo kidogo cha polisi huko Bunju.Tuliambiwa kuwa Dkt.Ulimboka alipatikana akiwa amepoteza fahamu na kuokotwa na msamaria mwema katika msitu wa Mabwepande jijini Dar-es-salaam na alikua ametokwa na damu nyingi sana. Waliomuokota ndio waliompeleka katika Kituo cha polisi Bunju.Tulipofika kituo cha polisi Bunju tuliweza kumchukua tukiwa na madaktari wenzie na hatimaye kwa sasa anaendelea na matibabu katika taasisi ya mifupa Muhimbili(MOI),
Kutokana na unyama huu na vitendo hivi vya kutweza utu wa mtu, Kituo cha Sheria na Haki a Binadamu na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania(THRD-Coalition), kwa niaba ya asasi zote zenye kujali haki za binadamu na watu binafsi watetezi wa Haki za Binadamu, kwa nguvu zetu zote na kwa uwezo tulionao, na kwa kumaanisha tunalaani kwa dhati kitendo hiki cha kumtesa na kumuumiza Dkt. Ulimboka ambacho hakikubaliki katika jamii ya kistaarabu.

Tunatoa tamko lifuatalo,

a) Kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

i. Kwanza watoe matibabu yanayofaa kuokoa maisha ya Dkt Ulimboka;
ii. Kufanya uchunguzi wa dhati wa tukio hili zima ;
iii. Kuwakamata wale wote waliohusika na tukio hili na wakala wao na kulitaarifu taifa kuhusu watu hao na sababu za kufanya jambo hili ovu lililomletea madhara makubwa Dr.Ulimboka;
iv. Na kwa weledimkubwa kuwatia hatiani na kuwashtaki wote waliohusika
v. Na kuhakikisha wahusika hao wanapata adhabu kali watakapotiwa hatiani.

b) Kwa Jeshi la Polisi:

- Kuacha kuwa na upande wowote katika mgogoro unaoendelea kati ya madaktari na serikali;
- Kuheshimu utawala wa sheria, haki za binadamu, kutomchukulia mtu kama ana hatia kabla haijathibitishwa na kuwa na weledi katika yote wanayoyatenda;

c) Kwa watetezi wa haki za Binadamu:
- Kujenga na kuendeleza mshikamano wetu katika ngazi zote na kulaani vitendo vya ushambuliaji kama hivi.

d) Kwa Wataalamu wa Tiba:
- Kutokana na mazingira chokozi yaliyopo yanayoweza kuleta hali hasi, tunazidi kuwasihi wanataaluma wote wa afya kujizuia kutolumbana moja kwa moja kwa wakati huu bali kuendelea kufuatilia haki zao kwa kufuata utaratibu wa kisheria.

e) Kwa Wananchi /umma wa watanzania,
- Kuunga mkono shughuli zote zinazofanyika katika kutafuta haki zinazohusiana na tukio hili
- Kudai uwajibikaji na maboresho ya huduma za kijamii hasa hasa huduma za afya Tanzania.
- Kulaani vitendo vyote kama hivi vinavyokiuka haki za binadamu.

Hivyo basi, yote aliyotendewa Dr. Ulimboka ni mlolongo wa makosa ya jinai kwa waliotenda hivyo. Zaidi ya hapo tukio hili linaonyesha uvunjwaji wa haki za msingi uliofanywa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama zinavyolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 vifungu vifuatavyo: 12, 13, 14, 15,16,17,18, 20, 22,23 na 29.

Tunaamini kuwa vitendo kama hivi huwa vinafanywa kwa makusudi ili kunyamazisha na kuzuia kazi na juhudi za watetezi wa haki za binadamu. Havipaswi kurudiwa tena katika nchi hii iliyostaarabika tena ya kidemkrasia kwani hili ni tishio la wazi kwa watetezi wote wa haki za binadamu Tanzania.

Imetolewa Dar-es-salaam Tanzania leo tarehe 27 Juni 2012.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
Dr. Helen Kijo-Bisimba

 Mratibu Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRD-Coalition)
Onesmo Olengurumwa

No comments:

Post a Comment