K |
atibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, amemteua Naibu Katibu Mkuu anayemaliza muda wake, Dkt, Asha-Rose Migiro kuwa mjumbe wake maalum katika masuala ya ukimwi na ugonjwa wa ukimwi Barani Afrika.
Ban Ki Moon ametangaza uteuzi huo wakati wa hafla maalum aliyoiandaa mahsusi kwaajili ya kumuaga Naibu Katibu Mkuu wake,ambaye anahitimisha utumishi wake wa miaka mitano na nusu katika nafasi ya Unaibu katibu Mkuu.
Hafla hiyo imefanyika siku ya alhamisi katika viunga vya Umoja wa Mataifa, na kuhudhuriwa na wageni waalikwa mbalimbali wakiwamo mabalozi na wakuu wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa.
Akiongea kwa hisia, Ban Ki Moon, ameeleza kwamba ingawa Migiro alikuwa naibu katibu mkuu wake, lakini amekuwa mwalimu wake, amejifunza mengi toka kwake na daima ataendelea kuenzi mchango wake mkubwa.
Amemuelezea Migiro kama kiongozi si tu mwadilifu, lakini mwanadiplomasia aliyebobea, aliyefanya kazi kubwa,ngumu na nzito kwa moyo mkunjufu, uhodari , umakini, na uadilifu wa hali ya juu sana.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akatumia fursa hiyo kuishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kumruhusu Migiro kwenda kuitumikia jumuia ya kimataifa.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu dkt. Asha-Rose Migiro amesema anaupokea kwa mikono miwili uteuzi wa kuwa mjumbe maalum wa Katibu Mkuu katika masuala ya Ukimwi.
Amemshukuru Ban Ki Moon, kwa kumuamini kwamba anaweza kumsaidia kama naibu Katibu Mkuu, na akamshukuru pia kwa ushirikiano mkubwa na uhusiano mkubwa uliojengeka kati yake na Ban Ki Moon lakini pia kati yake na wasaidizi wake. Ushirikiano ambao anasema ulichagiza utendaji kazi kufanikisha dira na matarajio ya Katibu Mkuu.
Hafla hiyo pia imehudhuriwa na familia ya Naibu Katibu Mkuu ikijumuisha mume wake, Profesa Cleophas Migiro, mdogo wa Naibu Katibu Mkuu, Bi. Amina Mtengeti na mtoto wa mwisho wa Migiro Chansa Jasmin.
Naibu Katibu Migiro anakuwa mwanamke wa pili kushika wadhifa huo na mwanamke mwafrika wa kwanza. Lakini pia ni naibu katibu mkuu ambaye amehudumu katika wadhifa huo kwa miaka mitano na nusu.
No comments:
Post a Comment