Tuesday, June 12, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: DK. KASHILILAH ASEMA BADWEL ATAENDELEA KUTAMBULIWA KAMA MBUNGE KWA ADHABU YA KIFUNGO CHINI YA MIEZI 6


K
ATIBU wa Bunge Dk. Thomas Kashililah ametoa ufafanuzi kuwa mbunge wa Bahi, Omar Badweli anayetuhumiwa kwa rushwa ataendele kuwa mbunge hata kama atahukumiwa kifungo cha chini ya miezi sita jela.
Dk. Kashililah amesema hayo jana alipozungumza kwa njia ya simu kuwa mbunge huyo bado ni mtuhumiwa na pia kwa mujibu wa katiba atakoma kuwa mbunge kama atahukumiwa kifungo cha kuanzia miezi sita jela.

Amesema hayo baada ya mbunge huyo Badwel kufunguliwa kesi mahakamani ya tuhuma ya kuomba rushwa ya sh. milioni nane toka halmashauri ya wilaya ya Mkuranga, Pwani.

Dk. Kashililah ametoa mfano wa mbunge wa Mbarali, Modestus Kilufi ambaye hivi karibuni mahakama ilimtia hatiani kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno kwa kukusudia na kumuhukumu kwenda jela miezi 10 au kulipa faini ya Sh. 500,000.
    
Hata hivyo Kilufi alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na mahakama ya Mbeya.
Alisema hata kama Badwel atafungwa kifungo cha chini ya miezi sita kwa mujibu wa katiba ataendelea kuwa mbunge atakapokuwa amemaliza kifungo chake hicho.

Ubunge wake utakoma tu endapo atafungwa zaidi ya miezi sita na hii ni kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema kumekuwa na kesi nyingi za kupinga matokeo ya uchaguzi katika maeneo mbalimbali lakini bunge huchukua maamuzi pale mahakama inapomaliza hukumu yake.

No comments:

Post a Comment