Wednesday, June 13, 2012

ABIDAL KUHUDHURIA MCHEZO KATI YA UFARANSA NA SWEDEN JIJINI KIEV.

BEKI wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Barcelona, Eric Abidal ambaye alifanyiwa upasuaji wa kupandikiza ini April mwaka huu anatarajiwa kusafiriki kuelekea jijini Kiev kuhudhuria mchezo baina ya timu ya taifa ya nchi yake na Sweden. Rais wa Shirikisho la Soka la Ufaransa, Noel Le Graet aliwaambia waandishi wa habari kuwa alimpatia mwaliko mchezaji huyo ambaye anatarajiwa kusafiri kutoka jijini Barcelona na kutua Kiev tayari kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo wa kundi D. Abidal mwenye umri wa miaka 32 alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe katika ini lake mwaka uliopita lakini baada ya kurejea uwanjani alilazimika kufanyiwa tena upasuaji wa kubadilisha ini ambalo alipewa na binamu yake April 10. Madaktari waliomfanyia upasuaji mchezaji huyo wamesema kuwa upasuaji huo hauwezi kumfanya mchezaji kushindwa kucheza soka tena. Abidal ameichezea timu ya taifa ya ufaransa michezo 61 na alikuwa sehemu ya kikosi cha nchi hiyo kilichomaliza katika nafasi ya pili ya michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2006 na pia alikuwemo kwenye kikosi kilichoshiriki ichuano ya euro 2008 pamoja na Kombe la Dunia mwaka 2010.

No comments:

Post a Comment