Monday, June 25, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: TAARIFA YA CHANJO YA MANJANO YAPOKELEWA NCHINI


W
izara ya Afya na Ustawi wa Jamii imepokea taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuhusu chanjo ya homa ya manjano kwa wasafiri kutoka Tanzania kwenda Jamhuri ya Kisoshalisti ya Sri Lanka. 

Taarifa hii imetolewa naUbalozi wa Jamhuri ya Sri Lanka uliopo Afrika ya Kusini ambayo inaeleza utaratibu mpya wa ukaguzi   na ufuatiliaji wa wasafiri katika Viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Bandaranayake, Katunakaye na Colombo nchini Sri Lanka. 

Kila msafiri anayeingia Sri Lanka atatakiwa kuwa na kadi ya chanjo ya homa ya manjano kama sharti la kiafya la kuingia nchini humo. Madhumuni ya utaratibu huu ni kudhibiti kuingia kwa ugonjwa wa homa ya manjano nchini Sri Lanka.

Kwa kuzingatia sharti hili muhimu,Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inawajulisha kuwa wasafiri wote wenye umri zaidi ya mwaka mmoja (1) wanatakiwa siku tisa (9) kabla ya kuingia nchini SriLanka wawe wamepata  chanjo ya homa ya manjano. 

Utaratibu huu pia,utawahusisha wasafiri wanaopita nchini Sri Lanka ambao watakuwa wanasubiri usafiri wa kwenda nchi nyingine.

Aidha, kwa wale wasafiri ambao hawastahili kuchanja chanjo hiyo kutokana na sababu za msingi za kiafya kama vile wasafiri wenye umri chini ya mwaka mmoja (1), wazee wenye umri zaidi ya miaka sitini (60), wajawazito, waathirika wa virusi vya UKIMWI na wenye matatizo mengine ya kiafya watatakiwa kuonyesha uthibitisho kutoka kwa daktari.

Wizara inapenda kuwataarifu wasafiri wote wanaosafiri kwenda au kupitia Sri Lanka kuzingati sharti hilo muhimu ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.

 Vile vile, ku hakikisha unapata chanjo hiyo katika vituo vinavyotambuliwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Kwa maelezo zaidi kuhusu ugonjwa wa homa ya manjano na utaratibu wa chanjo yake wasiliana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

REGINA L. KIKULIKAIMU KATIBU MKUU
25. 06. 2012

No comments:

Post a Comment