Wednesday, June 6, 2012

MWAMICHEZO BORA KULAMBA DOLA 8,000.

Add caption
MWANAMICHEZO Bora wa Tanzania kwa mwaka 2011 anatarajiwa kupewa dola za Marekani 8,000 (Zaidi ya sh. Milioni 12 za Tanzania) imetangazwa leo. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam leo, Meneja Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Imani Lwinga alisema uamuzi wa kutoa fedha una lengo la kumpa uhuru mshindi aweze kufanya mambo anayoyapenda kutokana na zawadi hiyo. “Nia ya kutoa zawadi ni kumfanya mshindi aone ana kitu fulani amepata, hivyo safari hii tumeona tutoe kiasi hicho cha fedha ambacho tunaamini kitakuwa changamoto kubwa kwa mshindi,” alisema Lwinga. Alieleza kuwa walipokea ombi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), ambacho ndiyo kinaandaa tuzo hiyo, kwamba safari hii kuwe na mabadiliko kwa mshindi akabidhiwe fedha badala ya zawadi ya gari kama ilivyokuwa mwaka jana. Pia mshindi huyo wa jumla atapewa cheti na kombe. Lwinga alisema pia Serengti itatoa zawadi ya Sh. Milioni moja kwa kila mshindi wa michezo mbalimbali ambayo itazawadiwa katika sherehe hizo zitakazofanyika Juni 14 mwaka huu ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam. Akizungumzia hilo, Katibu Mkuu wa TASWA, Amir Mhando alisema wanatarajia wanamichezo mbalimbali watapewa tuzo siku hiyo na kutaja michezo ambayo itapewa tuzo kuwa ni riadha, wavu,netiboli,kuogelea, tenisi, judo, kikapu, soka,ngumi za kulipwa, ngumi za ridhaa, gofu wa ridhaa, gofu wa kulipwa, baiskeli, kriketi. Mingine ni mpira wa mikono, olimpiki maalum, Mchezaji Bora wa Nje anayecheza Tanzania, Mchezaji Bora Chipukizi, Mchezaji Bora wa Tanzania anayecheza Nje, Karate, Mwanamichezo Bora wa Tanzania mwaka 2011 na Tuzo ya Heshima. Mhando ambaye pia ni Katibu wa Kamati ya Tuzo alisema Ijumaa watatangaza majina ya wanamichezo wote watakaowania tuzo hiyo na kuipongeza Serengeti kwa udhamini wao wa kila mwaka. Kwa mujibu wa Mhando mwaka 2006 Mwanamichezo Bora wa Tanzania alikuwa Samson Ramadhan aliyezawadiwa sh. 500,000, wakati mwaka uliofuata mshindi ambaye alikuwa Martine Sulle alizawadiwa Sh.500,000, huku mwaka 2008 mshindi akiwa Mary Naali alizawadiwa sh.750,000. Wote hao ni wanariadha.

No comments:

Post a Comment