Monday, July 2, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

PONGEZI KWA RAIS MPYA WA ZFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linampongeza Amani Ibrahim Makungu kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uchaguzi uliofanyika juzi (Juni 30 mwaka huu) kwenye hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar. Ushindi wa asilimia 94 alioupata Makungu ambaye hakuwa na mpinzani katika uchaguzi huo mdogo unaonesha imani ambayo wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA wanayo kwake katika kukiongoza chama hicho. Ni matarajio ya TFF kuwa ushindi huo utatafsiriwa kwa vitendo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa ZFA na wadau wa mpira wa miguu Zanzibar kwa kumpa Makungu ushirikiano wa asilimia 100 ili kuhakikisha Kamati yake ya utendaji inafanya kile kinachotarajiwa na wengi. Makungu si mgeni katika mpira wa miguu, na mchango aliotoa kwa mchezo huo visiwani kabla ya kuwania nafasi hiyo unatambuliwa na kila anayefuatilia maendeleo ya mpira wa miguu katika Zanzibar. TFF tunaahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ZFA chini ya Makungu kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake Ali Ferej Tamim ili kuhakikisha ustawi wa mpira wa miguu visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

MISRI YAAHIRISHA MECHI DHIDI YA NGORONGORO HEROES
Mechi mbili za kirafiki kati ya timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) na Misri zilizokuwa zichezwe mwezi huu zimefutwa. Chama cha Mpira wa Miguu Misri (EFA) kimetuma taarifa jana (Julai 1 mwaka huu) kikiomba kusogezwa mbele hadi mwishoni mwa Agosti baada ya kushindwa kupata usafiri wa ndege kuwahi tarehe ambazo ilikubaliana na TFF kwa ajili ya mechi hizo. Ngorongoro Heroes ambayo tayari iko kambini ilikuwa icheze mechi hizo Julai 3 na 5 mwaka huu jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi kabla ya kuikabili Nigeria katika mechi ya michuano ya Afrika, Julai 29 mwaka huu. Mechi nyingine za kirafiki kwa Ngorongoro Heroes inayofundishwa na Jakob Michelsen zitachezwa Julai 14 na 16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.

RUVUMA YAIFANYIA MAUAJI LINDI 7-2
Timu ya Ruvuma imethibitisha kuwa mwiba mkali katika michuano ya Copa Coca-Cola mwaka huu baada ya leo asubuhi (Julai 2 mwaka huu) kuishushia Lindi kipigo cha mabao 7-2. Hadi mapumziko kwenye mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa Uwanja wa Nyumbu mkoani Pwani, washindi ambao kwa matokeo hayo wamejiweka katika nafasi nzuri ya kucheza 16 bora walikuwa mbele kwa mabao 3-0. Waliotikisa nyavu ni Anthony Christian dakika ya 23 na 50, Edward Songo dakika ya 27, 75 na 86 na Sunday Leonard dakika ya 32 na 60. Mabao ya Lindi yalifungwa na Salum Mnyamwile dakika ya 18 kwa njia ya penalti na lingine dakika ya 48 kupitia kwa Mwarami Maundu. Nayo Tanga imepata ushindi wake wa kwanza katika michuano hiyo baada ya kuifunga Manyara mabao 2-0 katika mechi ya kundi B iliyochezwa Uwanja wa Tamco mkoani Pwani. Mabao ya washindi yalifungwa na Mbwana Musa dakika ya 47 na Issa Mwanga dakika ya 60. Katika mechi tatu zilizotangulia Tanga ilitoka sare ya mabao 3-3 na Morogoro, ikapata sare nyingine ya 1-1 dhidi ya Mwanza, na baadaye 1-1 na Tanga. Kagera imeendelea kujitutumua katika michuano hiyo baada ya kupata ushindi wake wa pili katika kundi D kwa kuilaza Kusini Unguja bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe jijini Dar es Salaam. Bao lake lilifungwa dakika ya 76 na Novati Sebastian. Mechi iliyopita Kagera iliifunga Tabora mabao 2-0 baada ya kuteleza katika mechi mbili za kwanza kwa kufungwa na Kilimanjaro na Singida. Mechi nyingine ilichezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam ambapo Kinondoni iliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mara.

UONGOZI TWIGA STARS WATOA TAMKO
Uongozi wa Twiga Stars umekana kuwepo vitendo vyovyote vya kinyume na maadili kwa wachezaji wa timu hiyo ambayo hivi karibuni ilitolewa kwenye mechi za mchujo za michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC). Wakizungumza na waandishi wa habari leo (Julai 2 mwaka huu), Meneja wa Twiga Stars, Furaha Francis na aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo Charles Boniface Mkwasa wamesema hakuna vitendo vya aina hiyo. Mkwasa amesema alikaririwa vibaya kuhusu suala hilo wakati akiwa kwenye mahojiano na kituo cha televisheni cha Star Tv kutokana na swali alilokuwa ameulizwa kuhusiana na vitendo hivyo. “Ukifuatilia mahojiano yangu na Star Tv mimi sikusema kuwa kuna vitendo hivyo. Tatizo nadhani lilianzia kwa magazeti yaliyonukuu kupitia Star Tv, na wala kujiuzulu kwangu hakukuhusiana na hilo, nimewajibika kama kocha kutokana na kutolewa na Ethiopia,” amesema Mkwasa. Naye Furaha Francis amesisitiza kuwa hakuna vitu vya aina hiyo katika timu hiyo, na kama kuna mtu ana ushahidi na hilo ni bora akauonesha badala ya kuzungumzia uvumi kuliko ukweli. “Ukweli ni kwamba si sisi na wachezaji tu ambao hatukufurahishwa kutolewa na Ethiopia, wapo Watanzania wengi ambao hawakufurahishwa na matokeo yale. Twiga Stars si timu ya kudumu, haikai na wachezaji kwa muda wote, kila mchezaji ana timu yake. “Madai yanayoenezwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu vitendo hivyo yametuchafua sana. Tunaomba kama kuna mtu ana ushahidi na hilo atueleze kuliko kuendelea kutuchafua,” amesema.

No comments:

Post a Comment