Wednesday, July 4, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: UNESCO YAKUBALI OMBO LA TANZANIA KUHUSU SELOUS GAME RESERVES

Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO katika kikao chake cha 36 kinachoendelea (tarehe 24 June hadi 6 Julai 2012) katika jiji la Saint Petersburg nchini Russia imelikubali ombi la Tanzania la kuurekebisha mpaka wa Pori la Akiba la Selous, ambalo ni Eneo la Urithi wa Dunia, ili kuruhusu uchimbaji wa Madini ya Urani

Eneo linalohusika ni asilimia 0.8 ya eneo la Pori la Akiba la Selous

Kwa mara ya kwanza ombi hilo lilipelekwa kwa Kamati hiyo ya Urithi wa Dunia ya UNESCO mwezi Januari 2011 ambapo lilijadiliwa katika Kikao chake cha 35 ambacho kilihamishia mjadala huo katika Kikao cha 36 kinachoendelea.

Uamuzi huo ulifanyika ili kuruhusu Tathmini ya Athari ya Mazingira (EIA) kukamilishwa na kutoa muda kwa wataalam wa IUCN kufika eneo linalihusika ili kuliona na kuhakiki taarifa ya tathmini hiyo.

Pori la Akiba la Selous ambalo lina ukubwa wa Kilomita za Mraba 50,000 ni mojawapo ya hifadhi kubwa duniani zenye viumbe mbalimbali. Ni eneo maarufu kwa nyanda kubwa za tambarare zenye nyasi na misitu ya miombo pamoja na aina nyingi za wanyamapori.

Kufuatia kukubaliwa kwa ombi hilo la nchi yetu nachukua fursa hii kutoa shukrani kwa Kamati ya Urithi wa Dunia, IUCN, Kituo cha Urithi wa Dunia na taasisi mbalimbali, pamoja na watu binafsi ambao walichangia katika kulifanya ombi letu kukubaliwa.

Uamuzi uliotolewa na Kamati ya Urithi wa Dunia utatupatia uwezo na fursa nzuri ya kutimiza malengo yetu kiuchumi na kijamii kwa wananchi. Pia tutapata uwezo wa kulihifadhi na kuliendeleza vyema zaidi Pori la Akiba la Selous.

Mhe Khamis Suedi Kagasheki
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII
4 Julai 2012

No comments:

Post a Comment