Tuesday, July 3, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: MAONI YA KATIBA ZANZIBAR

IMEELEZWA kuwa, dola yoyote duniani, haiwezi kupata ufanisi bila ya kuwepo ushirikiano mzuri miongini mwa wanajamii husika.

Kauli hiyo imetolewa na Richard Rimo, mjumbe wa tume ya kukusanya maoni juu ya rasimu ya kuundwa kwa Katiba mpya ya Tanzania wakati akizungumza na wakaazi wa shehia ya Kibuteni Mkoa wa Kusini Unguja. Rimo amewataka wakaazi wa shehia ya Kibuteni kutoa maoni yao kwa uwazi zaidi ili kufikia lengo la kuundwa kwa tume hiyo, sambamba na kuwahakikishia kuwa watayafanyia kazi kadiri itavyowezekana.

Mapema akitoa ufafanuzi, Mwenyekiti wa mjadala katika mkutano huo Muhammed Yussuf Mshamba alisema kuwa mchakato wa Katiba ni muhimu sana kwani maoni hayo yataonesha kuwa wananchi ndio wamiliki wa katiba hiyo. Aidha alisema Tume ya mabadiliko ni huru na haiwazuii wananchi kutoa maoni yao kwani ndio lengo la kuundwa kwake, lakini aliwaomba kuzingatia sana heshima ili waweze kufikia lengo linalokusudiwa.

Miongoni mwa wachangiaji, Rajab Haji aliiambia Tume hiyo kuwa Katiba itakayoundwa izingatie haja ya kuwa na wagombea binafsi wa Ubunge, Udiwani na Uwakilishi na kuondokana utaratibu wa sasa wa kutoa fursa kwa wagombea wenye vyama vya siasa tu sambamba na kuvitambua vikosi vya SMZ.

Pia alishauri Katiba ijayo izingatie kuwepo kwa mamlaka ya Watu wa Zanzibar na ile ya Tanganyika huru, pamoja na kutaka mgawanyo wa misaada kutoka nje itolewe sawa bila kuangalia ukubwa wa Tanzania bara. Aidha Haji alitaka Katiba mpya itoe umuhimu katika masuala ya elimu ya juu, Mafuta na gesi, akishauri kila upande wa muungano uwe na haki ya kuwa na mamlaka yake, jambo litakalotoa nafasi kuwepo kwa mamlaka ya Watu wa Zanzibar, na kutambuliwa hadhi ya Rais wa Zanzibar popote aendapo.

Mchangiaji Pandu Haji ( 48 ), alishauri kuwa Katiba mpya izingatie kuwa Tanzania ni Muungano wa nchi mbili hivyo ni vyema suala la ukusanyaji wa kodi liundiwe taratibu mpya kwa TRA kufanya kazi zake Tanzania bara pekee na sio Zanzibar. Hiyo, alisema itaipa mamlaka Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), kufanya kazi ya kukusanya mapato kwa uhuru ili yainufaishe Serikali ya Zanzibar na kuinua uchumi wake.

Zoezi la ukusanyaji wa maoni ya rasimu linalolenga kuandikwa kwa Katiba mpya ya Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, linaendelea vizuri, ambapo pia wachangiaji wengi wa Shehia ya Kibuteni waliwasilisha maoni yao kwa njia ya barua.

No comments:

Post a Comment