Wednesday, July 4, 2012

AFRICA NEWS: BURUNDI YAMTUNUKU TUZO MWALIMU NYERERE

Taifa la Burundi limemtunukia Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere Tuzo la juu kabisa ambayo Burundi hutoa kwa watu mbali mbali kutokana na mchango wao katika kuleta uhuru na baadaye kwa jitihada zao kubwa za kuleta amani katika nchi hiyo.

Mwalimu Nyerere ametunukiwa Tuzo hiyo inayoitwa 'Order of the National Republic of Burundi',  kwenye Kilele cha Sherehe za Kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi zizolifanyika leo, Independence Road, pembeni mwa Uwanja wa Michezo wa Louis Rwagasore mjini Bujumbura na kutangazwa hadharani kwa maelfu kwa maelfu ya watu waliohudhuria sherehe hizo. 

Tuzo hiyo ya Mwalimu imepokelewa kwa niaba yake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ambaye alikuwa mmoja wa viongozi sita wa nchi za nje waliohudhuria sherehe hizo.

Akitangaza Tuzo hilo, Rais wa Burundi, Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza alisema kuwa Burundi imeamua kumtunuku Mwalimu Nyerere sababu mbili – moja ni ushauri wake muhimu sana katika kuleta uhuru wa Burundi kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji.

Pamoja na Hayati Mwalimu, aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela pia amepata tuzo hiyo. Mzee Mandela alichukua nafasi ya Mwalimu kama mpatanishi wa mgogoro wa Burundi kufuatia kifo cha Mwalimu mwaka 1999.

Katika sherehe hizo, zilizoendelea mfululizo kwa saa saba unusu tokea saa nne asubuhi hadi saa 11 jioni, Rais Kikwete aliungana na viongozi wenzake wa nchi sita na wawakilishi wa nchi nyingine nyingi duniani kuhudhuria kilele cha sherehe za kufana kuadhimisha Miaka 50 ya Uhuru wa Burundi.

Burundi ilipata uhuru kutoka kwa wakoloni wa Kibelgiji Julai 2, mwaka 1962 na Rais Kikwete aliwasili Bujumbura asubuhi ya jana, akitokea Kigali, Rwanda, ambako pia alihudhuria sherehe kama hizo Kuadhimisha Sherehe za Miaka 50 ya Uhuru wa Rwanda iliyopata uhuru Julai Mosi, 1962, kutoka kwa wakoloni hao hao wa Kibelgiji.

Tofauti na Rwanda ambako Rais Kikwete alikuwa rais pekee aliyehudhuria sherehe za uhuru wa nchi hiyo na mgeni rasmi, katika sherehe za Burundi, Mheshimiwa Rais na Mama Salma Kikwete wameungana na Rais mwenyeji Pierre Nkurunzinza, Rais Mwai Kibaki wa Kenya, Rais Theodore Obing Nguema wa Equatorial Guinea, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Rais Francois Bozize wa Jamhuri ya Afrika ya Kati na Rais Shariff Sheikh Ahmed Shariff katika kusherehekea uhuru wa Burundi. 

Walikuwepo wawakilishi wa nchi nyingine nyingi duniani akiwamo Makamu wa Rais wa Uganda na Makamu wa Rais wa Nigeria, Mheshimiwa Prince Philip ambaye ni mtoto wa Malkia wa Belgium, Waziri Mkuu wa Swaziland na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) anayemaliza muda wake, Mheshimiwa Jean Ping.

No comments:

Post a Comment