Thursday, July 5, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: VYAMA NDANI YA KANISA KUKAGULIWA


Wizara ya Mambo  ya Ndani ya Nchi,  itaanza zoezi la kutembelea na kuhakiki Vyama vya Kijamii ambavyo  vimesajiliwa na Wizara hiyo ili kuhakikisha kuwa vyama hivyo vinafanya shughuli zake kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya Usajili wa Vyama.Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Sheria na Usajili wa Vyama vya Kijamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Numbilya Mpolo amesema kuwa zoezi hilo litaanza mwezi Agosti mwaka huu.


Akizungumza katika Banda la Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam ambapo Maonyesho ya 36 ya Biashara ya Kimataifa yanaendelea, Mpolo alisema mambo yatakayokaguliwa ni uhai wa Vyama hivyo na utekelezaji wa Katiba zake kama zilivyosajiliwa.Mambo mengine yatakayokaguliwa ni kama Vyama hivyo vinalipa ada ya kila mwaka kwa mujibu wa Sheria, na pia utekelezaji wa matakwa ya Sheria ya kufanya vikao vya Chama na kuandaa taarifa za fedha ambazo zinapaswa kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama kila mwaka.

Amesema hatua za kisheria zitachukuliwa kwa vyama vitakavyobainika  kukiuka masharti ya Sheria za uendeshaji wake, ikiwa ni pamoja na kupewa notisi za kusudio la kufuta chama husika.Kwa mujibu wa Sheria za Vyama, chama kitapewa notisi ya kusudio ya kukifuta, na ikiwa hakitatoa hoja kwa nini kisifutwe, ndani ya siku 21, basi Msajili wa Vyama anaweza kutoa notisi ya kukifuta chama, na baadaye kutoa tangazo la kukifuta chama hicho, katika Gazeti la Serikali.Akizungumzia kuhusu malalamiko yanayopokelewa na Msajili wa Vyama, Mpolo amesema ni pamoja na taarifa za migogoro inayotokana na kugombea madaraka na pia ubadhirifu wa fedha katika baadhi ya vyama.

Kuhusu Vyama ambavyo vinabadilisha Katiba zao bila mabadiliko hayo kukubaliwa na Msajili, amesema Katiba kama hizo hazitambuliki kisheria.Amesema hadi sasa  jumla ya Vyama vya Kijamii 6,469 vimesajiliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kati ya hivyo 875 ni Taasisi za kidini.Amesema zoezi la kusajili Vyama vya Kijamii bado linaendelea na wananchi wenye mahitaji ya kusajili hivyo wanaweza kuwasiliana  na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wowote ili kupata huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment