Thursday, July 5, 2012

OMAN HATARINI KUFUNGIWA NA FIFA.

OFA

NCHI ya Oman huenda ikaenguliwa katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe ya Dunia 2014 pamoja na kufungiwa mechi za kimataifa baada ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kukiri kuwa lina wasiwasi na amri ya mahakama iliyotolewa kubatilisha uchaguzi wa Chama cha Soka cha nchi hiyo-OFA. Katika taarifa yake FIFA wamesema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya shirikisho hilo pamoja na timu ya taifa kama matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwaka jana chini ya usimamizi wao wenyewe pamoja na Shirikisho la Soka barani Asia-AFC yatafutwa. Uwezekano wa kufutwa kwa matokeo hayo umekuja kufuatia amri ya mahakama iliyotolewa Juni 25 mwaka huu baada ya vilabu vitatu kulalamika na mazingira yaliyoendeshwa uchaguzi huo kuwa sio halali. Taarifa hiyo pia imesema kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa uhuru pasipo kuingiliwa na chombo chochote kingine hususani mahakama katika maamuzi yao. Oman sasa inaingia katika mzunguko wa mwisho wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Brazil mwaka 2014 kwa upande wa bara la Asia ambapo mpaka sasa wamekusanya alama mbili katika michezo mitatu waliyocheza na timu za Japan, Australia na Iraq.

No comments:

Post a Comment