Samuel Eto'o. |
KLABU ya Anzhi Makhachkala ya Urusi ambayo imetumia mamilioni kuhakikisha inamsajili mshambuliaji nyota wa kimataifa wa Cameroon Samuel Eto’o na kocha Guus Hiddink kutoka Uholanzi wamefungiwa kucheza michuano ya Ulaya katika uwanja wao wa nyumbani msimu huu. Klabu hiyo imemuandikia barua rais wa shirikisho la Soka Ulaya-UEFA, Michel Platini kuonyeshwa kusikitishwa kwake na kushangazwa na hatua ya shirikisho hilo kuwanyima haki ya kucheza michezo ya nyumbani ya Ligi ya Ulaya au Europa League katika uwanja wao wa nyumbani. UEFA ambao kwa mujibu wa barua walioandika Anzhi walifanya uamuzi huo kutokana na matatizo ya kiusalama lakini walipotafutwa ili kutoa ufafanuzi kuhusu suala hilo hawakupatikana mara moja. Mkurugenzi Mkuu wa klabu hiyo Aivaz Kaziakhmedov amesema kuwa amesikitishwa na hatua hiyo ya UEFA kuwafungia kutumia uwanja wao wa nyumbani katika michuano hiyo kwani wamekuwa wakiutumia katika michezo Ligi Kuu ya nchini humo kwa zaidi ya miaka 20 lakini hakuna tukio lolote lililosababisha maafa lililotokea uwanjani hapo. Mkurugenzi huyo aliendelea kusema kuwa mmiliki wa klabu hiyo ameweka fedha nyingi katika kuukarabati uwanja na kuwa wa kisasa katika mji huo, shule ya soka kwa vijana wadogo na pamoja na viwanja saba vya mazoezi na kuhoji watafanya nini na miradi yote hiyo iliyowekwa. Anzhi itaingia katika michuano hiyo kwenye hatua ya pili ya kufuzu na wanatarajiwa kukutana na mshindi kati ya timu ya Flamutari ya Allbania au Honved ya Hungary.
No comments:
Post a Comment