MHASIBU MKUU wa Halmashauri ya wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya Fedinand Nanyele anakabiliwa na shutuma za ubadhilifu wa fedha za miradi zaidi ya Sh. Milioni 100.
Taarifa za uchunguzi zilizothibitishwa na baadhi ya idara nyeti za Serikali zilisema kuwa mwasibu huyo baada ya kuhusishwa na ubadhilifu huo alikamatwa na kuhojiwa na taasisi ya kuzuia na kupamba na rushwa mkoani Mbeya na anatarajia kufikishwa mahakamani hivi karibuni.
Mbali na Mhasibu huyo, tuhuma hizo pia zinamhusu aliyekuwa Mkurugenzi wa wilaya hiyo George Kagomba ambaye ndiye alikuwa msimamizi mkuu wa matumizi ya fedha hizo za miradi ya Afya na ujenzi wa majengo ya Sekondari wilayani humo.
Akithibitisha tuhuma hizo, Kamanda wa Takukuru mkoa wa Mbeya Daniel Mtuka alisema kuwa ni kweli taasisi yake ilimshikilia na kumhoji mhasibu huyo na sasa jarada lake tayari limepelekwa kwa Mkurugenzi wa mashitaka (DPP).
Alisema tuhuma zinazowakabili viongozi hao ni ubadhilifu wa miradi ya Maendeleo ya wilaya hiyo ambapo kuna dosari zilizojionesha katika upande wa mfuko wa Afya na Elimu ambapo kwa upande wa Afya pekee Sh. Milioni 101 hazionekani zimeenda wapi na upande wa elimu Sh. Milioni 127.
Uchunguzi zaidi umebaini kuwa fedha za mfuko wa Afya zinaonekana kutotumika vema katika Hospitali ya Mission ya Chimala na fedha za elimu kupitia mfuko wa Capitation Fund zilitakiwa zitumike vema katika ujenzi wa vyumba vya madarasa eneo la Ubaruku na rujewa.
Mbali na viongozi hao, Takukuru imewahoji baadhi ya vigogo wa Halmashauri ya wilaya ya Ileje na inatarajia kuwahoji wengine kutoka wilaya za Mbeya, Chunya, Mbozi, Kyela na Jiji la Mbeya kwa tuhuma mbalimbali ambapo Kamanda Mtuka alisema kuwa ni mapema mno kufafanua jambo hili bali watakapokuwa tayari wamewahoji atatoa taarifa.
No comments:
Post a Comment