Monday, June 25, 2012

MBEYA UPDATE: AFISA MTENDAJI ATIMULIWA


A
FISA mtendaji wa Kijiji cha Nsalala kilichopo wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya Alihakimu Mjagaje ametimuliwa kazi na wananchi wa Kijiji hicho kwa ubadhilifu wa fedha na kukwamisha maendeleo ya kijiji hicho.

Mtendaji huyo aliamuliwa na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mwishoni mwa Juma kukabidhi mihuri na nyaraka muhimu papo hapo kwa kile walichosema kuwa wamechoka naye na wakaomba ajitete ambapo mtendaji huyo alishindwa kujitetea na hatimaye akaomba radhi na kuandika barua ya kurejesha fedha za kijiji ambazo alitakiwa kuzikabidhi.

Akifungua mkutano huo, mbele ya kikosi kazi cha mtandao wa www.kalulunga.blogspot.com ambacho kilialikwa kwa ajili ya kuhudhuria mkutano huo, Mwenyekiti wa Kijiji hicho Ezekiel Mwasenga alisema kuwa yeye binafsi amejaribu kumfichia mambo mengi mtendaji huyo lakini amefikia kikomo na kuutangazia umma kuwa hayupo tayari kufanya kazi naye.

Mwenyekiti huyo alisema kuwa kwa muda mrefu mtendaji huyo amekuwa mtoro katika ofisi yake huku akitumia mali ya ofisi ikiwemo mihuri kujinufaisha binafsi na pindi kamati za kijiji hicho zinapopanga utekelezaji wa miradi yeye hataki huku akitumia vibaya fedha za ruzuku za kijiji hicho kwa kujilipa posho.

Mbali na Mwenyekiti huyo, wajumbe wa Serikali ya Kijiji nao walisema kuwa hawako tayari kufanya kazi na Afisa mtendaji huyo ambapo waliungwa mkono na wananchi wa kijiji hicho na kwamba Mtendaji huyo amekaa katika kituo hicho kwa miaka sita bila faida kwa wananchi.

Sanjali na agenda hiyo, pia kulijitokeza suala la ujambazi ambalo walisema kuwa limeshika kasi katika kijiji hicho ambapo waliazimia watu wote wanaojihusisha na ujambazi katika kijiji hicho kuuawa kabla ya kutoa taarifa kwa viongozi wa Serikali.

Wakati wanatoa maazimio hayo, pia mkutano huo ulimwamuru Mwenyekiti wa Kijiji hicho kumwandikia Mwananchi mmoja waliyemtaja kwa jina la Kado barua ya kuondoka katika Kijiji hicho kwa madai kuwa anajihusisha na uhalifu na wakawaonya baadhi ya viongozi wa dola wanaotaka kuthubutu kumgeuzia kesi mwananchi mwenzao Hamis anayedaiwa kujeruhiwa na Nondo na Kado.

Kwa sasa kijiji hicho cha Nsalala kinakabiliwa na matatizo kadhaa likiwemo suala la ubovu wa shule ya Msingi Nsalala ambapo walidai kuwa suala hilo limekuwa tete kutokana na ukwamishwaji uliotokana na Afisa Mtendaji waliyemtimua kazi.

No comments:

Post a Comment