Friday, June 1, 2012

LAMPARD AONDOLEWA TIMU YA TAIFA.



KIUNGO wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Chelsea, Frank Lampard ameondolewa katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo kitakachoshiriki michuano ya Ulaya kutokana na kupata majeraha wakati wa mazoezi ya timu hiyo. Habari ya kuondolewa kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 33 zilitangazwa baada ya madaktari wa timu hiyo kumfanyia vipimo na kugundua kuwa hataweza kupona katika muda wa wiki moja iliyobakia kabla ya michuano hiyo. Kiungo wa klabu ya Liverpool, Jordan Henderson ndio anatarajiwa kuitwa katika kikosi hicho kuja kuziba pengo la Lampard. Akihojiwa kuhusiana na taarifa hizo kocha wa Uingereza Roy Hodgson amesema kuwa ni pigo kubwa kumpoteza mchezaji huyo haswa baada ya kumkosa mchezaji mwingine mzoefu Gareth Barry mapema wiki iliyopita. Hodgson aliendelea kusema kuwa ukweli kwamba madaktari hawawezi kuhakikisha kuwa Lampard hawezi kucheza mchezo wowote katika hatua ya makundi inamaanisha kuwa hawana jinsi zaidi ya kutafuta mbadala wake katika sehemu ya kiungo. Kama Henderson ambaye ana miaka 21 akikubaliwa kuziba nafasi ya Lampard, Liverpool itakuwa ni klabu ambayo ina wachezaji wengi zaidi walioitwa timu ya taifa ya nchi hiyo wakiwa wachezaji watano pamoja na kuwa na msimu mbaya katika Ligi Kuu nchini humo.

No comments:

Post a Comment