Sunday, June 17, 2012

KOCHA WA POLAND ABWAGA MANYANGA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Poland, Franciszek Smuda amekuwa kocha wa kwanza kutangaza kuachia ngazi kufuatia nchi hiyo ambayo ni wandaaji wenza wa michuano ya Ulaya kutolewa katika michuano hiyo. Akihojiwa mara baada ya timu hiyo kutolewa Smuda amesema kuwa ana asilimia 100 kwamba safari yake ya kukinoa kikosi hicho imefikia mwisho kwani mkataba wake ulikuwa unaisha mara baada ya michuano hiyo kumalizika. Poland ilishindwa kufanikiwa kufuzu baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Jamhuri ya Czech katika mchezo wa kundi A uliochezwa jijini Wroclaw. Smuda mwenye umri wa miaka 63 ambaye alichukua mikoba ya kuinoa timu hiyo mwaka 2009 aliweka wazi kuwa tayari alifanya makubaliano na Shirikisho la Soka la Poland kwamba mkataba wake hautaongezwa baada ya michuano hiyo. Nahodha wa timu hiyo Jakub Blaszczykowski ambaye ndiye alifunga bao la kusawazisha dhidi ya Urusi katika mchezo wa pili anaamini kuwa mashindano hayo yamekuwa muhimu kwao kujifunza.

No comments:

Post a Comment