Saturday, June 2, 2012

MISRI KUIVAA MSUMBIJI BILA MASHABIKI.

TIMU ya taifa ya Misri inatarajiwa kuanza mchezo wake wa kwanza wa kutafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil wakati watakapoikaribisha Msumbiji mchezo ambao utachezwa bila ya mashabiki kutokana na sababu za kiusalama. Mabingwa hao wa zamani wa Afrika wamecheza michezo mingi ya kirafiki ili kuwaweka wachezaji wake katika hali nzuri toka Ligi Kuu ya nchi hiyo ilipofutwa kufuatia vurugu zilizotokea Port Said na kupelekea watu kufa. Katika baadhi ya michezo ya kirafiki ambayo timu hiyo inayonolewa na Bob Bradley imecheza ni pamoja na mchezo dhidi ya Nigeria ambao walicheza jijini Dubai na kufanikiwa kuwafunga mabao 3-2 pia walizifunga timu za Cameroon mabao 2-0 na Togo mabao 3-0. Kwa upande wa Msumbiji wenyewe wamecheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Namibia uliochezwa Ujerumani kabla ya kuelekea Cairo Jumanne. Misri inatarajiwa kumkosa mchezaji wake mkongwe Ahmed Hassan ambaye alipata majeruhi wakati wa mazoezi ya timu hiyo ambayo imeweka kambi jijini Alexandria.

No comments:

Post a Comment