Friday, June 22, 2012

MBEYA UPDATE: WAJAWAZITO KUPATA HUDUMA YA NHIF/CHF


M
FUKO wa Taifa wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kanda ya Nyanda za juu kusini, umesema kuwa umeanza kuwawezesha wanawake wajawazito wasio na uwezo kupata matibabu chini ya utaratibu wa Bima ya Afya na Mfuko wa Afya ya Jamii CHF katika mkoa wa Mbeya kupitia mradi mpya wa KFW.

Akizungumza katika semina iliyojumuisha waandishi wa habari na waratibu kutoka katika Hospitali mbali mbali kutoka wilaya za mkoa wa Mbeya leo, Meneja mfawidhi wa mfuko huo kanda hiyo Celestin Muganga alisema kuwa mradi huo wa miaka miatu umefadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani na utakamilika ifikapo mwaka 2014.

Muganga amesema kwa mkoa wa Mbeya ulianza kufanyiwa majaribio katika wilaya za Ileje na Rungwe lakini tayari mradi umefika wilaya za kyela na Mbeya vijijini.

Ameutaja utaratibu wa kujiunga na mradi huo kuwa kigezo kikubwa cha kuwa mwanachama ni mwanamke aliyethibitika kuwa ni mjamzito na atahudumiwa kwa kipindi chote cha ujauzito wake na miezi mitatu baada ya kujifungua hapo ndipo kadi yake itakuwa imeisha.

Kwa upande wake Mganga mkuu wa mkoa wa Mbeya Sefu Mhina alisema kuwa mradi huo kupitia mfuko wa jamii (CHF) utafanikiwa sana kwa mkoa huo kutokana na kuanza kipindi cha mavuno ambacho wananchi wengi wanakuwa na ahueni ya kiuchumi.

Naye mganga ufuatiliaji wa ubora wa huduma za Bima ya Afya  Dr. Sam Nixon amesema kuwa kwa sasa wanufaika wa mfuko wa bima ya Afya wananufaika kwa kutibiwa na kupewa dawa aina 693 ambazo zina majina yake ya asili tofauti na zile zenye majina mawilimawili na kwamba bima ya Afya haitoi matibabu kwa magonjwa ya akili, vidonge vya kifua kikuu, ARVS, Ukoma, urembo na magonjwa yatokanayo na uvunjifu wa sheria.

Naye afisa mwingine wa mfuko huo wa bima ya Afya Tuli Mwakyusa, alitoa ufafanuzi kuwa watumishi ambao wamestaafu wanatakiwa kufika katika ofisi za mfuko wa bima ya Afya na kurejesha vitambulisho vyote ambapo watapatiwa fomu zingine na kupewa vitambulisho viwili na kwamba wategemezi hawatapatiwa vitambulisho vingine.

Akihitimisha semina hiyo Celestin Muganga amewaomba watoa huduma kutojihusisha na udanganyifu wa kujaza fomu na kuwapigia debe baadhi ya wauza dawa ambapo kwa sasa umejitokeza mtindo wa watoa huduma kuwaelekeza wagonjwa sehemu ya kuchukua dawa maduka ambayo yameonekana kuwa yana uhusiano wa kimaslahi na baadhi ya watoa huduma katika Hospitali zilizomo kwenye mpango wa bima ya Afya.

Kwa sasa Bima ya Afya inakabiliwa na mwamuko mdogo wa waratibu na watumishi wengine wa Serikali kuhamasisha wananchi kujiunga na mifuko ya NHIF na CHF jambo ambalo linapaswa kuangaliwa na Serikali na wadau mbalimbali wa masuala ya Afya zikiwemo asasi zisizokuwa za Serikali.

No comments:

Post a Comment