Friday, June 15, 2012

MBEYA UPDATE: MAUAJI MBEYA YAFIKIA 600 KWA 2011


Imeelezwa kuwa zaidi ya watu 600 waliuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira kali walioamua kujichukulia sheria mkononi katika kipindi cha mwaka jana pekee. 

Hayo yamesemwa na Wakili na Afisa wa ufuatiliaji wa Haki za Binadamu kutoka katika kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Laetitia Ntagazwa wakati akitoa mada kwenye mafunzo ya waangalizi wa Haki za Binadamu wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yaliyofanyika Jijini Mbeya. 

Amesema utafiti uliofanywa na LHRC umeonyesha kuwa katika kipindi cha mwaka jana pekee watu zaidi ya 600 wameuawa kwa kupigwa na wananchi, hali ambayo inaashiria kuwa vitendo vya watu kujichukulia sheria mkononi vinazidi kukithiri nchini. 

Aidha, Ntagazwa amesema  kufuatia kuongezeka kwa vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha sheria za nchi na ukiukwaji wa haki za Binadamu, Kituo cha Haki za Binadamu kimeamua kuchukua hatua ya kushirikiana na Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa wananchi juu ya athari za kujichukulia sheria mkononi. 

Amesema miongoni mwa mambo ambayo LHRC kinataka kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi ni kampeni ya utii bila Shuruti, ambapo wameamua kuwashirikisha Polisi kila mahali wanapokwenda kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waangalizi wa haki za binadamu.
Imeandikwa na Angella Sulluci, Mbeya

No comments:

Post a Comment