Sunday, June 24, 2012

MAZEMBE WAOMBA MCHEZO DHIDI YA AL AHLY UCHEZWE NJE YA MISRI.


 

MABINGWA wa zamani wa Afrika, klabu ya TP Mazembe imeliandikia Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF kuhamisha mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa barani humo dhidi ya klabu ya Al Ahly kuchezwa nje ya Misri. Mazembe wamefikia kuiandikia CAF barua hiyo kuhamisha mchezo huo kutokana na kutokuwa na imani kuhusu suala la usalama nchini humo. Katika taarifa hiyo ambayo pia waliituma katika mtandao wa klabu hiyo imesema kuwa kutokana na hali kuwa tete nchini Misri kutokana na uchaguzi wa rais wa nchi hiyo na kuvunjwa kwa bunge ndio sababu haswa zilizopelekea kuiomba CAF ihamishe mchezo huo uchezwe katika nchi nyingine yoyote ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea. Ofisa Mkuu wa Al Ahly, Sayed Al Hafez ameonyesha kukasirishwa na kitendo cha Mazembe kudai mchezo huo uhamishwe hiyo sio sahihi kwani wao walikuwa wanataka mchezo huo uchezwe jijini Cairo baada ya Uwanja wa Kijeshi wa nchi hiyo kukubaliwa kuchezwa mechi. Hafez amesema kuwa itakuwa sio sahihi kama mchezo huo ukiamishwa haswa ikizingatiwa kuwa wao walicheza mechi nchini Mali ambapo kulikuwa na wanajeshi wanaopigana na kupelekea baadhi ya msafara wa timu hiyo kuzuiwa nchini humo kwa siku sita. Mbali na yote hayo Hafez alimalizia kuwa wataheshimu maamuzi yoyote yatakayotolewa na CAF kuhusiana na mchezo huo ambao unatarajiwa kupigwa Julai 8 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment