Monday, June 18, 2012

EPL NEWS: MAN CITY NA MAN UTD KUKUTANA DESEMBA 8 ETTIHAD


M
ABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya England, Manchester City watafungua kampeni ya kutetea taji lao kwa kuumana na klabu iliyopanda msimu huu ya Southampton.

Mahasimu wa City, Manchester United wenyewe wataanza kampeni zao kwa kupimana ubavu na Everton, katika ufunguzi huo unaotarajiwa kufanyika Agosti 18 mwaka huu.

Reading iliyorejea Ligi Kuu, itakuwa na kazi ya ziada katika ufunguzi huyo itakapocheza Stoke City, wakatika ambapo Wagonga Nyundo wa London West Ham watatoana ngeu na Aston Villa.

 Pambano la mahasimu wa jiji la Manchester, linalosubiriwa kwa hamu limepangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Etihad jijini humo hapo Desemba 8, kabla ya kurudiana kwenye Uwanja wa Old Trafford Aprili 6 mwakani.

Kocha mpya wa Wekundu wa Anfield Liverpool, Brendan Rodgers ataanzia harakati za kuirejeshea klabu hiyo heshima kwa kuwafuata West Brom, inayonolewa na kocha wa zamani wa ‘Reds’, Steve Clarke.

Liverpool, ambayo ilikuwa na msimu mbaya uliopita chini ya Kenny Dalglish, imejikuta ikipangwa kuanzia nyumbani dhidi ya timu ngumu za Manchester City, Arsenal na Manchester United, kabla ya kuzifuata ugenini mzunguko wa pili.

Washika Bunduki wa London Arsenal, watanzia nyumbani kwa kuwaalika wageni wao Sunderland na mechi ya kwanza kwa Roberto Di Matteo kama kocha rasmi wa Chelsea ambao ni mabingwa wa Ulaya kwa kucheza na Wigan, huku Tottenham wakipangwa kuanza na Newcastle.

London derby inayohusisha mahasimu wa jiji hilo itaanzia kwa Chelsea kuwafuata Arsenal hapo Septemba 29, kabla ya Gunners tena kuvaana na mahasimu wao wengine Tottenham hapo Novemba 17 kwenye Uwanja wa Emirates.

 Kwa mujibu wa ratiba ya FA, Manchester City wataumana na Norwich nyumbani katika hitimisho la msimu, huku majirani zao Man United wakiwafuata West Brom. Chelsea itamaliza na Everton kwenye dimba la Stamford Bridge, huku Arsenal ikitarajiwa kumaliza na Newcastle.

No comments:

Post a Comment