Saturday, June 9, 2012

ADEBAYOR KUIKOSA DRC.


 

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Togo ambaye alikuwa akicheza kwa mkopo katika klabu ya Tottenham Hotspurs akitokea Manchester City, Emmanuel Adebayor kwa mara nyingine atakosa mchezo baina ya timu yake ya taifa itakayocheza dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC utakaofanyika jijini Kinshasa Kesho. Kocha wa Togo Didier Six kutoka Ufaransa alimjumuisha mchezaji huyo katika kikosi kilichocheza na Libya na kutoa sare ya bao 1-1 wiki iliyopita lakini hakutokea katika kikosi hicho. Shirikisho la Soka la Togo-FTF limesema kuwa Adebayor hajawasiliana nao kujua tatizo lake pamoja na kufanya nae mazungumzo wiki chache zilizopita kuhusu suala la kurejea katika kikosi hicho. Pamoja na hayo FTF imesema kuwa bado wataendelea kufanya mazungumzo na mchezaji huyo ili aweze kurejea katika kikosi hicho kwasababu wachezaji wenzake wanamuhitaji na taifa linauhitaji mchango wake. Adebayor alistaafu kuchezea timu ya taifa ya nchi hiyo Januari mwaka 2010 kutokana na tukio la ugaidi lililotokea kwa basi la timu hiyo kushambuliwa wakati wakielekea katika michuano ya Mataifa ya Afrika huko Cabinda, Angola lakini alirejea tena Novemba mwaka jana.

No comments:

Post a Comment