Wednesday, June 6, 2012

TANZANIA YAPAA KATIKA VIWANGO VYA FIFA.

TANZANIA imepanda katika viwango vya ubora vinavyotolewa na Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA pamoja na Taifa Stars kupoteza mchezo wa kutafuta tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia 2014 dhidi ya Ivory Coast uliofanyika jijini Abdijan wiki iliyopita. Katika viwango hivyo ambavyo vimetolewa leo na FIFA Tanzania imekwea mpaka nafasi ya 139 ikiwa imepanda kwa nafasi sita kutoka nafasi ya 145 waliyokuwepo mwezi uliopita. Mbali na Tanzania katika orodha mabingwa wa soka wa Ulaya na Dunia Hispania wameendelea kushikilia usukani katika orodha wakifuatiwa na Uruguay ambao wamechukua nafasi ya Ujerumani walioshuka hadi nafasi ya tatu. Nafasi ya nne katika orodha hiyo inashikiliwa na Uholanzi wakati nafasi ya tano inashikiliwa na mabingwa wa mara tano wa michuano ya Kombe la Dunia Brazil ambao mwezi uliopita walikuwa katika nafasi ya sita ambayo sasa nafasi hiyo imechukuliwa na Uingereza. Nchi zingine ambazo zipo katika kumi bora ya orodha hiyo ni pamoja na Argentina ambao wamepanda kwa nafasi mbili huku Croatia wakiwa wamebakia katika nafasi yao ya nane wakifuatiwa na Denmark ambao wamepanda nafasi moja na kumi bora inafungwa na Ureno ambao wameporomoka kwa nafasi tano. Kwa upande wa Afrika Ivory Coast bado wanaendelea kuongoza pamoja na kudondoka kwa nafasi moja katika orodha hiyo na kuangukia nafasi ya 16 wakifuatiwa na Ghana ambao wako nafasi ya 25 nao wakiwa wameanguka nafasi tatu wakati Algeria wanakuwa watatu wakiwa katika nafasi ya 32 wakiwa wamepanda nafasi nne. Nafasi ya nne katika tano bora za Afrika inashikiliwa na Libya ambao wamepanda nafasi nne mpaka nafasi ya 42 huku nafasi ya tano inashikiliwa na Mali ambao wameporomoka kwa nafasi nne pamoja na mabingwa wa soka Afrika Zambia ambao nao wameshuka kwa nafasi tatu hivyo wote wanafungana katika nafasi ya 43.

No comments:

Post a Comment