Thursday, June 14, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: WABUNGE WALIA NA BAJETI 2012/2013


WENYEVITI wa vyama vya Chadema, NCCR Mageuzi na CUF wameiponda Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2012/2013 iliyowasilishwa bungeni jana na Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa wakisema imeongeza mzigo kwa walipa kodi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa Serikali.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kuwasilishwa kwa bajeti hiyo jana, wenyeviti hao walisema hakuna matumaini kwa Watanzania kupitia Bajeti hiyo kwani fedha nyingi zimerundikwa kuwanufaisha wachache huku umma ukiambulia patupu.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Hakuna mkataba wa makusudi wa kupunguza matumizi ya Serikali, ahadi yake ya kupunguza matumizi kwa kupunguza posho zisizo na tija na matumizi mengine haikutekelezwa.” Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, amesema ameshangazwa na kutokuwapo kwa nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma na badala yake fedha nyingi kurundikwa katika matumizi ya kawaida ya Serikali. Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema matatizo makubwa katika bajeti hiyo ni kutengwa kwa fedha kidogo za maendeleo na kwamba kinachoshangaza ni Serikali kushindwa hata kugharimia matumizi ya kawaida. Mwenyekiti wa NCCR Mageuzi, James Mbatia alisema Serikali lazima ijifunze kubadilika kwani kilichotangazwa jana kwenye Bajeti yake ni marudio ya miaka yote.

Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka amesema Bajeti hiyo kama zilivyo nyingine,  imeendelea kujikita katika kuongeza kodi katika bidhaa zilezile kila mwaka. Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Ester Bulaya amesema Bajeti hiyo ni nzuri akipongeza mkakati wa ukarabati mkubwa wa Reli ya Kati.

No comments:

Post a Comment