Monday, June 11, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: MAMIA WAMWAGA BOB MAKANI


R
AIS Jakaya Kikwete ameongoza mamia ya waombolezaji kutoa heshima za mwisho kwa mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bob Makani (76), aliyefariki dunia Jumamosi iliyopita.

Akizungumza katika shughuli hiyo, iliyofanyika kwenye Viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam, Rais Kikwete amesema mchango wa hayati Makani hasa katika nyanja za kisiasa na kiuchumi utakumbukwa daima na Watanzania.


Katika hotuba yake fupi, Rais ameeleza jinsi alivyozipata taarifa za msiba huo mkubwa na jinsi alivyoguswa kwa kumpoteza mwanasiasa mkongwe....

Akimzungumzia hayati Makani, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema alikuwa ni mwanasiasa mahiri na mkweli, lakini mfumo wa kisiasa Tanzania haukumpa fursa ya kupata nafasi ya uongozi kitaifa.

Amesema, Makani aligombea ubunge zaidi ya mara mbili lakini hakuwahi kushinda kwa kile ambacho Mbowe alidai kuwa ni tatizo la mfumo.

Katika hotuba yake, Mbowe alimkumbuka nyakati muhimu za marehemu Makani alizowahi kuzishuhudia ikiwemo kutoa hotuba fupi kuliko zote katika moja ya kampeni zake za kugombea ubunge huko Shinyanga.

Kwa upande wake Mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei aliyeanzisha chama hicho pamoja na Makani amesema taifa limepoteza nguzo imara wakati huu likiwa katika mchakato wa mabadiliko muhimu ya nchi.

Hotuba hiyo ya Mtei iliyosomwa kwa niaba yake na Mzee wa Chadema, Victor Kimesera ilieleza historia ya wawili hao wakiwa wanafunzi katika Shule ya Sekondari Tabora na baadaye wafanyakazi wa BoT.

Naye Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amemtaja marehemu Makani kuwa mtu jasiri ambaye alianzisha chama cha upinzani hasa enzi zile ambazo upinzani ulionekana kama uhaini... “Alikuwa ni mtu ambaye haogopi, alisema hadharani kile alichokiona kinafaa.”

Dk Slaa amesema japokuwa Makani alikuwa mgonjwa na umri wake kuwa mkubwa, lakini bado aliendelea kufanya kazi za chama bila makosa.

No comments:

Post a Comment