Wednesday, June 6, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: CHADEMA YAMNASA KADA WA CUF


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilizindua vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika Mkoa wa Lindi huku kikimtaka Mbunge wa Jimbo la Lindi Mjini (CUF), Salum Barwani kujiunga na chama hicho.
 FREEMAN MBOWE
Katika siku hiyo ya kwanza, Chadema kilimnasa aliyekuwa meneja wa kampeni wa mbunge huyo, Abdallah Madebe. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema mbunge huyo kwa sasa na wabunge wenzake wa CUF wamekuwa hawana sauti ya kutetea wananchi ndani ya Bunge kwa kuwa uongozi wa juu wa chama hicho umeungana na CCM.
Mbowe alimkaribisha mbunge huyo baada ya wananchi wa Kata ya Nng’apa, kusema Barwani amefuatilia baadhi ya malalamiko yao ya muda mrefu lakini, juhudi zake zinakwamishwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi na madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Lindi. Malalamiko mengine ya wananchi hao yalikuwa mfumuko wa bei, kukosa huduma za afya na wanafunzi kutozwa Sh20,000 kwa ajili ya ulinzi wa shule za Serikali. Mkazi wa Kata ya Ng’apa, Rashid Issa alimweleza Mbowe katika mkutano huo kuwa hajui hatima ya maisha yao kutokana na mfumuko wa bei unaojitokeza kila wakati huku wakiendelea kutozwa kodi katika vivuko vya mazao na fedha hizo kuishia mikononi mwa wajanja.

Akijibu hoja hizo, Mbowe alisema maisha magumu kwa Watanzania ni matokeo ya sera mbovu za Serikali ya CCM katika kusimamia uchumi wa nchi.

Akimzungumzia Barwani, Mbowe alisema katika mazingira ya sasa ya CUF, mbunge huyo hatakuwa na uwezo wa kuwasaidia wananchi kwa sababu viongozi wa juu wa chama hicho, akiwamo Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu, Seif Sharif Hamad ndiyo wanaofanya uamuzi na ‘wamekiunganisha’ chama hicho na CCM.
Mbowe aliwataka wakazi wa Lindi kutowavumilia viongozi wazembe ambao hawawezi kuwaelezea kodi zao zimetumika vipi, wakati wao wanashindwa kupata huduma za msingi.

No comments:

Post a Comment