Sunday, June 10, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: BOB MAKANI'S DEATH UPDATE


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimelazimika kukatiza ziara yake ya kujiimarisha katika mikoa ya kusini kutokana na kifo cha mwasisi wake, Bob Nyanga Makani, kilichotokea usiku wa kuamkia jana.
Tayari viongozi wakuu wote wa chama hicho wamerejea jijini Dar es Salaam, kushughulikia taratibu za mazishi ya mwanasiasa huyo, aliyewahi kushika nyadhifa kadhaa katika Serikali ya Awamu ya Kwanza. Akielezea msiba huo jana, Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa CHADEMA, John Mnyika, amesema kuwa wameupokea kwa majonzi makubwa kutokana na mzee huyo kuwa nguzo muhimu kwenye chama. Makani ambaye alikuwa katibu mkuu wa kwanza na mwenyekiti wa pili wa chama hicho, alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam saa 4.15 usiku, akisumbuliwa na maradhi ya kibofu cha mkojo na mapafu. Amesema kuwa CHADEMA itasonga mbele kutokana na kuamini katika falsafa ya utamaduni wa kupokezana vijiti, na kwamba mapambano yataendelezwa mpaka kieleweke. Afya ya mzee Makani ilianza kuzorota miaka ya karibuni ambapo, wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2010 katika viwanja vya Jangwani, aliishiwa nguvu na kudondoka aliposimama kuwasalimia wananchi.

Pia Januari 17 mwaka huu katika msiba wa aliyekuwa mbunge wa viti maalumu wa CHADEMA, Regia Mtema, Makani alianguka tena muda mfupi baada ya kuaga mwili wa marehemu. Mamia ya waombolezaji wakiongozwa na viongozi mbalimbali wa CHADEMA, jana walimiminika nyumbani kwa marehemu kuwafariji ndugu jamaa na marafiki.

Makani enzi za uhai wake aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa CHADEMA kuanzia mwaka 1993 hadi 1998, Mwenyekiti wa chama hicho kuanzia mwaka 1998 hadi 2004 na amegombea ubunge wa 2005.

No comments:

Post a Comment