Thursday, June 14, 2012

MBEYA UPDATE: WALI WASABABISHA FUJO RUNGWE


Jeshi la Polisi wilayani Rungwe Mkoa wa Mbeya linawashikilia wanafunzi zaidi ya 20 kwa makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanya fujo kwa kuvunja samani,madirisha na kuiba mali za shule ya Seminari Manow ya Wilayani Rungwe inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania-KKKT.
Wanafunzi hao wamehusika kufanya fujo katika shule hiyo Juni 14,2012 wakidai kutotendewa haki kwa kupikiwa ugali badala ya wali
  
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Masiba Watson amesema Mali zenye thamani ya jumla ya shilingi Milioni 50 zimeharibiwa zikiwemo Kompyuta,Madawati,Madirisha  na samani nyingine katika Shule hiyo

 Mmoja wa Wanafunzi hao amesema waliamua kugoma kutokana na uongozi wa shule kutengua 'ratiba ya wali' na kuwapikia ugali kwa madai kuwa mchele hautoshi katika hifadhi.

Awali Mkuu wa shule hiyo amesema juhudi za uongozi wa shule kuwataka wanafunzi hao watulie ziligonga mwamba kutokana na ghasia ambazo hazikuweza kutulizwa mapema hadi pale kikosi cha kutuliza ghasia-FFU kilipofika shuleni hapo na kutuliza fujo iliyokuwa ikifanywa na wanafunzi hao

Masiba ameongeza kuwa wanafunzi hao pia wamechana mitihani waliyokuwa waanze kuifanya Juni 15, ambapo karatasi za mitihani hiyo mara baada ya kuchanwa walizisambaza katika viunga vya shule hiyo

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Chrispin Meela ambaye alifika shuleni hap mara baada ya fujo kutokea amesema serikali ya wilaya ya Rungwe haijafurahishwa na kitendo cha kufanya fujo kilichotekelezwa na wanafunzi hao na kuonya kuwa sheria itachukua mkondo wake dhidi ya wanafunzi watakaobainika kuhusika na fujo hizo kwa namna moja au nyingine.

Kufuatia fujo hiyo Mkuu huyo wa Wilaya ameifunga Shule hiyo hadi tarehe pili mwezi Julai 2012 kwa kidato cha pili,tatu,nne na sita ambao wanaaminika kuwa sababu ya fujo hizo na kuwaagiza wanafunzi hao kuja shuleni hapo na wazazi wao kwa maelezo na barua.

No comments:

Post a Comment