Monday, June 11, 2012

MBEYA UPDATE: SERIKALI YAPEWA SIKU SABA KUKUSANYA NYARAKA ZA UCHOCHEZI


W
achungaji wa Madhehebu ya Kikristo,Wilaya ya Momba,Mkoani Mbeya wameipa siku saba Serikali kukusanya nyaraka za uchochezi nchini zinazoendelea kusambazwa na baadhi ya waumini wanaojiita wenye msimamo mkali wa dini ya kiislamu.
Tukio hilo limetokea juzi katika Ukumbi wa Kanisa la Kilutheli  Tanzania(KKKT) Usharika wa Tunduma na kujumuisha wachungaji,wainjilisti,walimu na mapadre wa madhehebu yote ya kikristo yaliyopo wilayani humo.

Mwenyekiti wa kikao hicho Gideon Neema Mwamafupa na Katibu wake Padre Isaac Mbanga,walipokea maoni kutoka kwa wachungaji walioongea kwa uchungu kufuatia Serikali kukaa kimya kutokana na matamko na usambazaji wa CD za uchochezi dhidi ya wakristo nchini na kwamba kitendo hicho wanakiona ni ukiukwaji wa haki za binadamu na kukiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha wachungaji wamesema Serikali imekiuka Ibara ya 50 ya katiba,kifungu cha 15 na 146 sura ya 4 kuhusiana na madaraka ya Umma,ambapo Serikali imeruhusu kujengwa misikiti katika vituo vya mafuta vya oil com nchini hali ambayo ni hatari kwa usalama.

Pia wamesema wamekerwa na kitendo cha wasomali kuzagaa katika mji huo,huku Maafisa wa polisi na uhamiaji wakiwaangalia tu wakiwa hawana kazi na hata Vibali vya kuishi nchini,lakini ifikapo saa saba huenda katika msikiti wa Oil Com na kufanya ibada.

Hata hivyo wamekuwa wakishinda katika baadhi ya nyumba za watanzania waliopo mpakani(Tunduma) na hivyo kutishia usalama wa taifa letu.

Wachungaji hao wamesema kuwa endapo Serikali haitatekeleza maagizo hayo wataipeleka mahakamani kwa sababu imeshindwa kusimamia Katiba na hii imetia wasiwasi hata kule Zanzibar kuchomwa kwa makanisa kunatia hofu usalama wao na kwamba kwa sasa hawapo tayari kunyanyasika tena


Mwisho walimaliza kwa kutoa tamko kuanzia Jumanne ya Juni 12 hadi 19 mwaka huu,kama hakuna hatua za makusudi kudhibiti hali hiyo wataandamana nchi nzima kudai haki zao.

Imeandikwa na Ezekiel Kamanga, Mbeya

No comments:

Post a Comment