Monday, June 11, 2012

MBEYA UPDATE: MTENDA KYELA RICE YATOA TZS 10 Mil. KWA WAKULIMA


MFANYABIASHARA na Mkurugenzi wa kampuni ya Mtenda Kyela Rice ya Mkoani Mbeya George Mtenda  ametoa msaada wa zaidi ya Shillingi million 10 kwa vikundi vya wakulima vitano vilivyopo Mkoani Mbeya mwishoni mwa juma lililopita.
Mtenda amevitaja vikundi ambavyo ameweza kuvisaidia fedha hizo kuwa ni Kamsamba, Kyela, Chitete na Lusungo vyote vya Mkoani hapa ambapo amekuwa akiviwezesha pia Mbegu bora na Mbolea ili vikundi hivyo viweze kupata chakula kingi kitakachowanufaisha wakulima na yeye kama mfanyabiashara.

Amesema kilichomsukuma kutoa fedha hizo kwa vikundi vya wakulima ni kutokana na umuhimu wa wakulima kwa wafanyabiashara hivyo amesema ni vyema kama mfanyabiashara akawawezesha wakulima kwa kuwapatia Mbegu, Mbolea na fedha ili waweze kupata chakula cha kutosha kitakachowanufaisha.

Amesema wafanyabiashara wanapaswa kuwekeza kwa wakulima kwa kuwa ndio watu wenye kila kitu chenye manufaa ya kibiashara hivyo na kudai kuwa bila hivyo hakuna mfanyabiashara ambaye anaweza kujivunia na biashara yake pasipo wakulima.

Akizungumza wakati wa mavuno ya mbegu alizowapatia wakulima katika kijiji cha Lusungo wilayani Mbeya juzi mtenda alisema mbegu alizowapatia wakulima hao aina ya Tan 250, Tan 254 na Tan H 600 za kampuni ya Tanseed International Ltd ndizo zitakazowanufaisha wakulima hao ili kwa kuwa yeye ndiye atakayezinunua kutoka kwao.

Amesema vikundi vya wakulima hao vitakuwa na uhakika wa kuuza bidhaa zao kwa kuwa soko tayari lipo na yeye ndiye mnunuzi wa mbegu hizo ndiyo maana anajitolea mbegu na Mbolea ili wakulima waongeze kipato chao kwa kupewa mbegu bora na zenye kuvumilia ukame hasa ukizingatia hali ya Mvua haitabiriki.

Katika mkusanyiko wa wakulima uliofanyika kijiji cha Lusungo, Mtenda aliwahidi wakulima Shillingi million moja ili waweze kujenga ghala la kuhifadhia mahindi wakati wanaposubiri mnunuzi na pia amewaomba wanakikundi cha Wekeza Upate Pembejeo (WEUPE) kuchagua watu wane ili waende kwenye maonyesho ya nane nane yatakayofanyika Mjini Dodoma kwa gharama zake.

Kwa upande wake mwenyekiti wa kikundi cha Weupe Sadick Kamwela alisema licha ya mbegu waliopewa na Kampuni ya Tanseed International Ltd kuchelewa kuipanda lakini mavuno waliyoyapata ni tofauti na wenzao ambao walitangulia kupanda mbegu aina nyingine mwezi mmoja kabla yao.
Naye mwakilishi wa kampuni ya Tanseed International katika kanda ya nyanda za juu kusini Happy Shuma alisema anawashukuru wakulima kwa kuzikubali mbegu za kampuni yao kwa kuwa wao wenyewe wakulima ndio waliweza kulima na kuzitathimini na hatimaye kuzikubali.

Aidha amesema mbegu hizo zina uwezo wa kutoa mavuno mengi na bora na kubainisha kuwa katika ekari moja mbegu aina ya Tan250 inazalisha kiasi cha magunia 16 -24 wakati Tan254 inatoa magunia kati ya 16-28 na Tan H600 inauwezo wa kutoa magunia 28-32.

No comments:

Post a Comment