Thursday, June 14, 2012

MBEYA UPDATE: CHADEMA KUTAKA KUZICHAPA KAVU


J
ESHI la polisi wilaya ya Mbeya likiongozwa na kamanda wa polisi wa wilaya hiyo wamezima mapigano yaliyokuwa yameratibiwa na chama hicho kwa ajili ya kumshusha jukwaani na kumpiga huku wakionesha mabango ya kutomtaka Mwenyekiti wa chama hicho wilaya ya Mbeya mjini John Mwambigija.

Hali hiyo imejitokeza leo katika mkutano wa hadhara uliokuwa unafanyika eneo la soko la Sido Mwanjelwa Jijini Mbeya.

Baada ya kuwepo taarifa za kupigwa kwa mwenyekiti huyo jeshi la polisi na vikosi vyake vilizingira mkutano na kusababisha baadhi ya wanachama wa chama hicho kuogopa kufanya kama walivyokuwa wamekusudia lakini wakashindwa kujizuia kuonesha mabango juu kuashiria kuwa hawamtaki kiongozi wao huyo.

Mabango hayo ambayo mengi walikuwa wameyakunja kuhofia kukamatwa na polisi, yalinyooshwa juu wakati alipopanda jukwaaani Mwambigija na kuanza kumwaga sera kama kikpindi cha kampeni huku akiendelea kupiga propaganda kuwa Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya aliwajengea vilabu wakazi wa Mbeya hali ambayo baadhi ya viongozi walichukizwa na kauli zake na kwamba akikamatwa hawako tayari kumsaidia.

Aidha alisema kuwa ''Waandishi andikeni ninachosema maana wengi hamuandiki ninachokisema mpaka aseme John Mnyika'' hali ambayo ilizidisha ukimya wa mkutano tofauti na mikutano mingine kama ilivyozoeleka.

Baadhi ya viongozi waliozungumza na mtandao wa kalulunga walisema kuwa wamechoshwa na tabia za Mwenyekiti huyo kukiharibu chama hicho na kuweka makundi huku akijitapa kuwa asingekuwa yeye Mbunge wa sasa Joseph Mbilinyi (SUGU) asingeweza kupita.

Viongozi hao wamesema kuwa kutokana na utisho wa askari polisi waliokuwepo katika mkutano huo watafanya mkutano wa ndani wa kumkataa na baada ya hapo watafanya mikutano ya hadhara kueleza udhaifu wa kiongozi huyo ndani ya chama hicho huku wakisema kuwa Katibu mkuu wa Chadema Taifa Dr. Wilbroad Slaa ndiye anayemlinda.

Kamanda wa polisi wa wilaya ya Mbeya Silvester Ibrahim alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema kuwa amesikitishwa na kauli za Mwambigija anapokuwa jukwaani licha ya kumwokoa lakini ameendelea kulitukana jeshi la polisi kana kwamba yupo katika jukwaa la kampeni badala ya kuelezea kuwa tangu wapewe Ubunge wamefanya nini.

Hivi karibuni mshauri wa chama hicho mkoa wa Mbeya Eddo Makatta Mwamalala alisema anasikitishwa na vyombo vya dola kuendelea kumwangalia kiongozi huyo anapotoa kauli za uchochezi anapokuwa jukwaani.

Hata hivyo Mwambigija alipohojiwa na kituo cha redio cha ROCK FM kilichopo Jijini Mbeya alikebehi madai ya kiongozi wake huyo huku naye Dr. Slaa akisema kuwa wanaojadili uchochezi wa Mwambigija wamefirisika kisiasa.


Mpaka tunaenda mitamboni imeelezwa kuwa chama hicho hasa viongozi wapo vipande vipande ambapo mpaka sasa Mwenyekiti wa vijana mkoa wa Mbeya ...Kasambala anajadiliwa baada ya kutoa kauli ya kukifedhehesha chama hicho katika mkutano wa hadhara kuwa chama hicho ndicho kilikuwa kimeratibu vurugu za Mwanjelwa zilizotokea hivi karibuni.

Mwambigija mbali na hali inayomkabili kwa sasa ndani ya chama huku kukiwa na tuhuma za ulaji wa fedha za ruzuku za chama hicho anadaiwa kuwatukana na kuwakejeli wapiga kura wa chama hicho eneo la Manga hasa wanawake kuwa watavaa nguo za kujisitiri wakati wa hedhi kwa miezi mitatu.....

Imeandikwa na Gordon Kalulunga, Mbeya

No comments:

Post a Comment