Tuesday, June 26, 2012

INGEKUWAJE KAMA MASHABIKI WA SOKA WANGEKUWA WATULIVU KAMA MASHABIKI WA TENISI.

Serena na Venus Williams.
NIMEKAA nyuma ya luninga yangu nyumbani nafuatilia kwa karibu mechi za ufunguzi wa michuano yenye historia ndefu na kusisimua katika mchezo wa tenisi duniani ya Wimbledon ambayo inafanyika jijini London, Uingereza.

Mchezo ambao unaendelea ni kati ya mchezaji ambaye kwasasa ndiye anashika namba moja kwa ubora duniani Novak Djokovic raia wa Serbia akimuhenyesha vilivyo Juan Carlos Ferrero kutoka Hispania kwenye mchezo huo.

Kwa kawaida mimi huwa ni mpenzi wa mchezo wa tenisi mbali na mchezo huo kinachonivutia zaidi ni utulivu wa mashabiki ambao huwa wanafuatilia mchezo huo pale uwanjani.

Kwani ni mara chache unaweza kuwasikia mashabiki hao wakipiga makofi pale mmoja wa wachezaji waliopo uwanjani kwa muda huo anapokuwa amepata alama kumshinda mwenzake na baada ya hapo hukaa kimya wakiendelea kufuatilia kwa makini mchezo. 

Mchezo unakwisha kwa Djokovic kusonga mbele katika michuano hiyo baada ya kufanikiwa kumfunga Ferrero kwa seti tatu yaani 6-3 6-3 6-1 ambapo mara baada ya mchezo mashabiki walipiga makofi kumpongeza mshindi na kuanza kuondoka kwa utulivu.

Hapohapo najikuta nikicheka mwenyewe nikikumbuka kelele za mashabiki wa soka wanapokuwa uwanjani ambazo zinakuwa zimechanganyika na kauli za kuudhi kwa mashabiki wenyewe, viongozi na hata wachezaji ambao wanawapa burudani mashabiki hao.

Mbali na hayo yote kitu kingine ambacho kimeonekana kama kinaota mizizi katika ligi nyingi barani Ulaya ni suala la ubaguzi wa rangi wa waziwazi wanaoonyesha mashabiki wa baadhi ya timu za huko kwa wachezaji ambao wana asili ya kiafrika.

Baadhi ya wachezaji ambao wamekumbwa na dhahma kama hiyo ni pamoja na mshambuliaji nyota wa Cameroon, Samuel Eto’o ambaye wakati anacheza katika klabu ya Barcelona ya nchini Hispania alitishia kujitoa uwanjani mpaka alipobembelezwa na wachezaji wenzie kuendelea na mchezo baada ya shabiki mmoja kurusha ndizi uwanjani.

Mwingine ni beki wa zamani wa Arsenal Emmanuel Eboue ambaye na yeye alikutwa na mkasa kama huo wakati alipohamia klabu ya Galatasaray ya nchini Uturuki, pia mshambuliaji wa klabu ya New York Red Bull ya nchini Marekani Thierry Henry naye yameshawahi kumtokea wakati akiwa nchini Uingereza katika klabu ya Arsenal.

Mlolongo wa matukio kama hayo ambayo wanafanyiwa wachezaji weusi ni mengi mno mpaka sasa na bado yanaendelea kitu ambacho ni nadra au naweza kusema hakuna kabisa katika mchezo wa kistaarabu kama tenisi.

Nathubutu kusema hivyo kwakuwa nimeshashuhudia mara kadhaa michezo inayowahusisha wachezaji wenye asili ya kiafrika hususani wadada wawili wanaotoka katika familia moja Venus na Serena Williams huwezi kusikia wakifananishwa na nyani au kutupiwa ndizi wakati wanacheza.

Tofauti na mchezo wa soka ambao hata katika michuano ya Ulaya ambayo inaendelea huko nchini Poland na Ukraine matukio ya vurugu na ubaguzi kwa wachezaji weusi kwa mashabiki yamekuwa kama ni jambo la kawaida.

Nadhani wakati umefika kwa mashabiki wa mchezao wa soka kuiga wenzao wa mchezo wa tenisi kushangilia kwa ustaarabu bila kukwazana vitendo ambavyo vimekuwa havina tija kwani mwisho wake vimekuwa vikisababisha usumbufu, uharibifu na hata vifo muda mwingine.

Ndio maana nikajiuliza hivi ingekuwaje mashabiki wa mchezo wa soka kama wangekuwa wastaarabu kama mashabiki wa mchezo wa tenisi?

Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment