Wednesday, June 20, 2012

BLATTER ASISITIZA UMUHIMU WA TEKNOLOGIA YA MSTARI WA GOLI.


 

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amerudia kauli yake ya kusisitiza mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli baada ya bao la utata lililofungwa wakati wa mchezo baina ya Uingereza na wenyeji Ukraine ambao uliisha kwa wenyeji kutolewa kwa bao 1-0. Shuti la mchezaji wa Ukraine Marko Devic lilionekana kuvuka mstari wa goli wakati wa mchezo baina ya timu hizo jijini Donetsk lakini mwamuzi alikataa bao hilo la kusawazisha kwa wenyeji. Utata wa bao hilo umekuja wakati ambapo mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli unatarajiwa kupitishwa na Bodi ya Kimataifa ya mchezo wa Soka-IFAB katika kikao chake cha Julai 5 mwaka huu. Mara baada ya mchezo wa huo Blatter aliandika katika ukurasa wa mtandao wake wa kijamii wa twitter kuwa mfumo huo kwasasa sio njia mbadala bali ni lazima uwepo ili kuondoa utata kama wa mechi ya jana. Lakini Blatter amesema kuwa anategemea mkutano wa IFAB utakaofanyika jijini Zurich, Switzerland utaweza kuruhusu mfumo mmojawapo kati ya miwili iliyopo uanze kutumika. Na ikiwa hivyo baadhi ya vyama vya soka vitaamua kuutumia au kutoutumia mfumo huo katika ligi zao. Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA, Michele Platini ambaye anapendelea zaidi watumike waamuzi watano katika mchezo badala ya mfumo huo anaweza asiutumie katika michuano ya shirikisho hilo.

No comments:

Post a Comment