Monday, June 25, 2012

BEKI WA ZAMANI WA LIVERPOOL AFARIKI DUNIA.

Miki Roque.
BEKI wa zamani wa Liverpool Miki Roque amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 23 jijini Barcelona, Hispania kufuatia kusumbuliwa na maradhi ya saratani. Beki huyo ambaye mpaka mauti yanamkuta alikuwa akikipiga katika klabu ya Real Betis alianza katika timu ya vijana ya Liverpool kuanzia mwaka 2005 mpaka 2009 na kufanikiwa kushinda Kombe la Vijana la FA mwaka 2006 kabla ya kujiunga na Betis. Amewahi kucheza mara moja katika kikosi cha kwanza cha Liverpool katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Desemba mwaka 2006 dhidi ya timu ya Galatasaray. Roque aligundulika kuwa na saratani mapema mwaka jana ambapo alifanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe katika fupanyonga lakini matibabu hayo hayakuzaa matunda kwani mchezaji huyo aliendelea kupambana na maradhi hayo mpaka mauti yalipomkuta Jumamosi iliyopita. Klabu ya Liverpool imetuma salamu za rambirambi kwa familia ya mchezaji huyo na kumuelezea kwamba alikuwa mchezaji kijana mwenye upendo na juhudi kubwa awapo uwanjani.

No comments:

Post a Comment