MWANASOKA bora wa dunia, Lionel Messi wa Barcelona amefanikiwa kufunga mabao mawili dhidi ya Real Zaragoza katika mchezo wa Ligi Kuu ya Hispania jana na kufikisha idadi ya mabao 60 msimu wa 2011-12 katika mashindano yote. Kijana huyo wa umri wa miaka 24, aliwafungia bao la kwanza mabingwa hao watetezi wa ligi hiyo maarufu kama-La Liga dakika ya 39 dhidi ya timu hiyo ambayo ilitangulia kupata bao kupitia kwa Carlos Aranda. Messi alifunga kutoka umbali wa mita 15 baada ya kupokea mpira kutoka kwa Alexis Sanchez na kuifanya Barca iongoze kwa mabao 2-1, ikiwa ni dakika tatu tangu Carles Puyol asawazishe. Bao la pili lilitokana na mkwaju wa penalti, zikiwa zimesalia dakika tano na kuifanya Barcelona iwe mbele kwa 3-1. Bao hilo la 60 la Muargentina huyo, linamfanya abakishe mabao saba tu kufikia rekodi ya Gerd Muller mchezaji anayeongoza kufunga mabao kwa msimu mmoja Ulaya. Mjerumani huyo, alitimiza mabao 67 akiwa Bayern Munich msimu wa 1972-1973.
Mabao ya Messi yanatokana na mabao 38 aliyofunga katika La Liga; mawili kwenye Kombe la Mfalme; matatu kwenye Supercopa, moja kwenye Super Cup ya UEFA; mawili Klabu Bingwa ya Dunia na mengine 14 katika Ligi ya Mabingwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment