skip to main |
skip to sidebar
 |
| Pele. |
MCHEZAJI nyota wa zamani wa Brazil, Pele amesema kuwa kikosi cha nchi hiyo ambacho kilinyakuwa Kombe la Dunia mwaka 1970 kilikuwa na wachezaji wengi wenye vipaji ukilinganisha na kikosi cha sasa cha Hispania ambacho kimefanikiwa kutetea taji la michuano ya Ulaya. Akiulizwa kuwa ni timu ingeshinda kati ya hiyo ya Brazil ya mwaka 1970 na Hispania ya hivi sasa nyota huyo wa zamani alijibu kwa kujiamini kwamba kama angekuwa anacheza isingekuwa na shaka kwamba wangeshinda mtanange huo. Hispania ambao wameshinda mataji mawili ya Ulaya mfululizo pamoja na lile la Kombe la Dunia 2010 imekuwa timu ya kwanza katika historia kushinda mataji matatu makubwa ya kimataifa. Ustadi wa kumiliki mpira ulioonyshwa na wachezaji wa Hispania na kuwasadia kutete taji lao hilo umefananishwa na ule wa kikosi cha Brazil cha mwaka 1970 ambacho kilikuwa na wachezaji kama Pele, Rivellino, Gerson, Tostao na Jairzinho ambao walinyakuwa Kombe la Dunia nchini Mexico kwa kuifunga Italia kwa mabao 4-1 katika mchezo wa fainali. Pele alistaafu kucheza soka mwaka 1971 na hakuwepo katika kikosi cha Brazil ambacho kilishiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1974 ambapo kilimaliza katika nafasi ya nne.
 |
| Sepp Blatter. |
MJADALA uliochukua karibu miaka kumi kuhusiana na suala la matumizi ya mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli katika mchezo wa soka unaweza kufikia tamati leo katika kikao cha Bodi ya Kimataifa ya mchezo wa Soka-IFAB kitakachokaa. Katika kikao cha leo ambacho kitafanyika katika makao makuu ya Shirikisho la soka duniani-FIFA ajenda kubwa itakuwa ni kuzijadili kampuni mbili ambazo mifumo yake imekuwa ikifanyiwa majaribio katika kipindi cha miezi kadhaa. Kutakuwa na kura nane katika kikao hicho cha IFAB ambapo kura nne zitakuwa za wajumbe wa FIFA na kura moja kwa kila nchi wanachama za Uingereza, Scotland, Wales na Ireland ya Kaskazini na kura zinazohitajika kupitisha mfumo mojawapo ni robo tatu ya kura zote. Rais wa FIFA, Sepp Blatter amekuwa akiwahimiza wajumbe wake kukubaliana na mfumo huo kufuatia tukio lililotokea katika michuano ya Ulaya mwaka huu ambapo shuti alilopiga mchezaji wa Ukraine Marco Devi kuonekana limeokolewa na beki wa Uingereza John Terry mpira ukiwa umevuka mstari lakini mwamuzi aliwanyima bao hilo. Mara baada ya tukio hilo Blatter aliandika ujumbe katika mtandao wa kijamii wa twitter kuwa suala la mfumo wa teknologia ya kompyuta katika mstari wa goli ni suala la lazima katika soka la kisasa. Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA yeye ameweka imani katika matumizi ya waamuzi watano katika mechi ambapo waamuzi wawili wanakuwa pembeni ya magoli nayo pia inaweza kupitishwa na IFAB leo.
 |
| OFA |
NCHI ya Oman huenda ikaenguliwa katika mechi za kufuzu michuano ya Kombe ya Dunia 2014 pamoja na kufungiwa mechi za kimataifa baada ya Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kukiri kuwa lina wasiwasi na amri ya mahakama iliyotolewa kubatilisha uchaguzi wa Chama cha Soka cha nchi hiyo-OFA. Katika taarifa yake FIFA wamesema kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya shirikisho hilo pamoja na timu ya taifa kama matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwaka jana chini ya usimamizi wao wenyewe pamoja na Shirikisho la Soka barani Asia-AFC yatafutwa. Uwezekano wa kufutwa kwa matokeo hayo umekuja kufuatia amri ya mahakama iliyotolewa Juni 25 mwaka huu baada ya vilabu vitatu kulalamika na mazingira yaliyoendeshwa uchaguzi huo kuwa sio halali. Taarifa hiyo pia imesema kuwa wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kufanya shughuli zao kwa uhuru pasipo kuingiliwa na chombo chochote kingine hususani mahakama katika maamuzi yao. Oman sasa inaingia katika mzunguko wa mwisho wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika nchini Brazil mwaka 2014 kwa upande wa bara la Asia ambapo mpaka sasa wamekusanya alama mbili katika michezo mitatu waliyocheza na timu za Japan, Australia na Iraq.