Thursday, July 5, 2012

MBEYA UPDATE: AJIRA 100 ZAMWAGWA NEW IMARA SECURITY


KAMPUNI ya New Imara Security yenye makao yake makuu Jijini Mbeya imemwaga ajira kwa watanzania 100 ambao wana mafunzo ya Kijeshi wakiwemo waliofuzu mafunzo ya Skauti.

Akizungumza jana na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Essau Kamwela alisema kuwa watanzania hao watafanya kazi katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara ikiwemo mikoa ya  ya Dar es Salam, Mbeya, Dodoma, Lindi, Iringa na Mtwara.

Mkurugenzi huyo alisema wenye mafunzo hayo wanaohitaji kazi ya ulinzi kupitia kampuni yake wajitokeze na si kwa kusema kuwa wanao uzoefu bali yeyote ambaye amepitia mafunzo ya Kijeshi na kustaafu katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), JKT, Polisi, Magereza na waliohitimu mafunzo ya Mgambo na Skauti.

Alisema kwa wenye nia ya dhati ya kufanya kazi hiyo ya ulinzi katika kampuni yake wafike katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo eneo la uwanja wa Sokoine Mbeya mkabala na benki ya NBC na wale waliopo mkoani Mtwara wafike katika ofisi za kampuni hiyo zilizopo eneo la Barabara ya Soko kuu na mkoani Lindi, Dodoma, Dar es Salaam, Iringa na Njombe wafike karibu katika matawi ya ofisi za kampuni hiyo.

Mkurugenzi huyo ametanabaisha kuwa lengo lake ni kuondoa tatizo la ajira kwa askari wastaafu na wenye taaluma hiyo ya kijeshi ambao watasaidia katika suala zima la ulinzi shirikishi na kujiongezea vipato vyao na familia.

Alisema watakaoajiriwa ni wale tu waliopitia mafunzo ya Jeshi la wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la kujenga Taifa (JKT), Polisi, Magereza na wale waliopita mafunzo ya jeshi la Mgambo na Skauti na waliowahi kufanya kazi na kustaafu huwa wanatakiwa kwenda na barua zao za kustaafu kwao ndipo watapata ajira.


Sanjari na hayo alitoa wito kwa wadau wa kampuni za ulinzi kuwa wanapopelekewa askari ambao wanamashaka nao, wanatakiwa kutoa taarifa kwa viongozi wa makampuni husika wanayoingia nayo mikataba ili kubadilishiwa walinzi kwa ajili ya usalama wa mali zao.

Kamwela ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama cha wamiliki wa makampuni ya ulinzi Tanzania Tanzania Security Industry Association (TSIA) kanda ya Nyanda za juu kusini Essau Kamwela, alisema jamii inapaswa kubadili fikra na dhana iliyojengeka ya kuwadharau askari wanaozitumikia kampuni hizo kwasababu walinzi hao bado ni askari wakakamavu sawa na walioko Serikalini.

No comments:

Post a Comment