skip to main |
skip to sidebar
 |
Clarence Seedorf. |
KLABU ya Botafogo ya nchini Brazil imekubali kumsajili kiungo wa kimataifa wa Uholanzi Clarence Seedorf ambaye ana umri wa miaka 36 kwa mkataba wa miaka miwili. Rais wa klabu hiyo Mauricio Assuncao alithibitisha ujio wa mchezaji huyo katika klabu hiyo baada ya taarifa kutoka katika mtandao wa klabu hiyo juu ya ujio wake. Assuncao amesema kuwa Seedorf haji nchini humo kwa ajili ya kufuata pesa bali ni changamoto katika soka la Brazil ndiyo zilizomfanya aje amalizie soka lake nchini humo hivyo hatua klabuni hapo kwa ajili ya matembezi. Seedorf ambaye mkataba wake na klabu ya AC Milan ya Italia ulimalizika mapema mwezi huu baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka 10, ameoa mwanamke wa kibrazil na mara kwa mara ameonekana akiwa katika mapumziko katika fukwe za jiji la Rio de Janeiro. Kiungo huyo ameshinda mataji mawili kati ya manne ya michuano ya Klabu ya Ulaya akiwa na Milan ambapo ni mmoja wa wachezaji wenye umri mkubwa katika klabu hiyo ambao wameondoka msimu wa majira ya kiangazi.
MABINGWA kihistoria Misri wameshindwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi Afrika ya Kati-CAR hivyo kuondolewa kwa jumla ya mabao 4-3 katika michezo miwili waliyocheza. Misri wanaikosa michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo chini ya kocha Bob Bradley ambaye alipewa kibarua cha kukinoa kikosi hicho mwaka uliopita baada ya kushindwa kufuzu michuano ya mwaka 2012. Katika mchezo wa kwanza baina ya timu hizo Misri ilijikuta ikifungwa katika uwanja wa nyumbani jijini Alexandria kwa mabao 3-2 na kuacha mshangao mkubwa miongoni mwa mashabiki wa timu hiyo. CAR imeingia katika mchujo ambao utajumuisha timu 30 ambazo zitacheza hatua ya mtoano ili kupata timu 15 ambazo ndio zitakazofuzu kushiriki michuano ya Mataifa ya Afrika mapema mwakani wakiungana na mwenyeji wa michuano hiyo Afrika Kusini.
 |
Ben Gordon. |
NYOTA wa mpira wa kikapu wa anayecheza katika Ligi Kuu ya mchezo huo nchini Marekani-NBA Ben Gordon ameenguliwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza baada ya kushindwa kuripoti katika kambi ya timu hiyo katika tarehe ya mwisho ambayo ilikuwa Juni 30 mwaka huu. Gordon ambaye anacheza katika klabu ya Charlotte Bobcats nafasi ya ulinzi alitajwa katika orodha ya wachezaji ambao watachujwa Aprili mwaka huu na kocha mkuu wa timu hiyo Chris Finch ambaye alikuwa akitegemea kumjumuisha katika kikosi chake cha mwisho. Kushindikana kutokea katika kambi hiyo kwa nyota huyo kumesababisha kikosi hicho kupwaya katika sehemu ya ulinzi na kupelekea kushindwa katika michezo yao mitano ya kujipima nguvu ambayo wamecheza wakiwa katika kambi waliyoweka huko Texas, Marekani. Gordon ambaye amejiunga na Bobcats akitokea timu ya Detroit Pistons mapema wiki hii amekuwa akijumuishwa katika kikosi cha Uingereza toka mwaka 2008 lakini hajawahi kucheza hata mchezo mmoja kutokana na majeruhi, matatizo ya kifamilia pamoja na majukumu mengine. Kikosi hicho kinatarajiwa kurejea nchini uingereza baada ya kushindwa mechi zake zote walizocheza nchini Marekani ukiwemo mchezo mmoja waliocheza na Nigeria na miwili katika kila timu za Lithuania na Urusi.