Tuesday, May 1, 2012

FERGUSON AMTUHUMU MANCINI KUWABUGUDHI WAAMUZI.

KOCHA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amemtuhumu kocha Manchester City Roberto Mancini kwa kuwasumbua waamuzi baada ya makocha hao kugombana wakati wa mchezo baina ya timu hizo ulichezwa jana. Ferguson na Mancini ilibidi watenganishwe baada ya kushindwa kuzuia jazba zao kwa kunyoosheana vidole dakika ya ya 76 ya mchezo huo ambao City walifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0. Ferguson alinyanyuka kutoka alipokuwa amekaa na kuanza kulalamika mchezo mbaya aliochezewa mshambuliaji wa timu yake Danny Welbeck na beki wa City Nigel De Jong. Kocha huyo ambaye ana miaka 70 alimtuhumu Mancini kuwabugudhi waamuzi katika kipindi chote cha msimu huu lakini akahoji kwanini kocha huyo hajalalamikia mchezo huo.

KOCHA WA MALI AREJEA BAADA YA MACHAFUKO KUTULIA.

KOCHA wa timu ya taifa ya Mali, Alain Giresse amerejea baada ya kuondoka na familia yake kutokana na machafuko ya kisiasa yaliyotokea nchini humo. Giresse mwenye umri wa miaka 59 anatarajiwa kusaini mkataba mpya baadae wiki hii na Shirikisho la Soka la nchi hiyo kufuatia mkataba wake wa awali ambao ulikuwa wa miaka miwili kuisha Februari mwaka huu. Kocha huyo alikiongoza kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo na kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ikiwa ni rekodi ya juu kabisa kuwekwa na nchi hiyo katika miaka 40 iliyopita. Taarifa zilizozagaa jijini Bamako zinasema kwamba kocha huyo ambaye ni raia wa Ufaransa atapewa mkataba wa mwaka mmoja ambapo mkataba huo unaweza kuongezwa kama timu hiyo ikifanikiwa kufuzu kucheza michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2014. Mali imepangwa katika kundi H ikiwa na timu za Algeria, Benin, na Rwanda ambapo June 6 mwaka huu inatarajiwa kucheza na Benin katika mzunguko wa pili kabla ya kuikaribisha Algeria jijini Bamako wiki moja baadae.

REDKNAPP AMKUBALI HODGSON KUINOA UINGEREZA.

MENEJA wa Tottenham Hotspurs, Harry Redknapp amesema kuwa haoni tatizo mpinzani wake Roy Hodgson kupewa kibarua cha kukinoa kikosi cha timu ya taifa ya Uingereza. Redknapp amekuwa akitajwa kukinoa kikosi hicho toka aliyekuwa kocha wa timu hiyo Fabio Capello alipojiuzulu wadhifa huo Februari ambapo Chama cha Soka cha Uingereza-FA kimeamua kuanza mazungumzo ya awali na Hodgson ambaye ni kocha West Bromwich Albion. Hodgson ambaye ana miaka 64 amewahi kushinda mataji nane ya ligi katika nchi mbili tofauti akiwa anafundisha vilabu vitatu tofauti ambapo pia amewahi kuzifundisha timu za Switzerland, Finland na Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE. Kocha huyo alikutana na viongozi wa FA jana katika mkutano uliochukua muda wa saa nne uliofanyika katika Uwanja wa Wembley jijini London. Redknapp amesema kuwa kwasasa anafurahishwa na kibarua chake katika klabu ya Tottenham na anamtakia mafanikio Hodgson kama atapewa kibarua cha kionoa timu hiyo kwani anaamini anaiweza kazi hiyo kutokana na uzoefu mkubwa aliokuwa nao katika soka ya kimataifa. FA inatarajiwa kumtangaza Hodgson kama kocha mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo baadae leo mbele ya vyombo vya habari.