Monday, June 4, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: WARATIBU WA SENSA WATAKIWA KUWA MAKINI ZOEZI LA SENSA

Ikiwa imebaki miezi michache kabla ya kuanza kwa zoezi la Sensa ya watu na makazi nchini serikali imewataka waratibu wa zoezi hilo kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu fedha na rasilimali zinazopelekwa kwenye mikoa na wilaya zote nchini ili kufanikisha zoezi hilo.

Akizungumza na waratibu wa Sensa ya watu na makazi 2012 kutoka katika mikoa na wilaya zote nchini leo mjini Morogoro naibu katibu mkuu Ofisi ya Waziri mkuu ,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw.Alphayo Kidata amesema kuwa zoezi hilo litafanikiwa kwa kiwango kikubwa kama waratibu hao watasimamia ipasavyo matumizi ya fedha na rasilimali zinazopelekwa katika meneo yao.

Amesema jukumu la usimamizi wa Sensa kwenye ngazi ya mikoa na wilaya ni la viongozi wa maeneo hayo na kufafanua kuwa kushindwa kwa zozei hilo katika wilaya au mikoa husika ni kiashirio cha viongozi hao kushindwa kusimamia majukumu yao kwani takwimu zitakazopatikana zitatumiwa pia na mamlaka za mikoa na wilaya katika shughuli za maendeleo.

Amefafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzbar ndio waratibu wa Zoezi hilo na Kufafanuz kuwa sensa ya watu na makazi kwa mwaka huu inalenga kupata takwimu sahihi ambazo zitasaidia kutunga Sera na kupanga programu za maendeleo za kuiwezesha serikali kupanga na kutathmini mipango ya maendeleo nchini.

Awali akizungumza kabla ya ufunguzi wa mkutano huo Mkurugenzi wa Sensa ya watu na Takwimu za jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Ephraim Kwesigabo amesema kuwa hivi sasa maandalizi yamekamilika na kuongeza kuwa mafunzo hayo ya awali kwa waratibu wa Sensa kutoka mikoa na wilaya zote nchini yanalenga kuwajengea uwezo waratibu hao ili waweze kusimamia vyema maeneo yao wakati wa zoezi la Sensa.

Naye Mratibu wa taifa wa Sensa ya watu na makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bw. Irenius Ruyobya amefafanua kuwa tayari maandalizi ya ufanikishaji wa zoezi la sensa ikiwemo upatikanaji wa vifaa vya kisasa kwa ajili ya zoezi hilo yamekwishafanyika.


No comments:

Post a Comment