Thursday, June 7, 2012

TANZANIA SOCIAL NEWS: LOWASSA ACHANGIA TZS 10 Mil.


WAZIRI Mkuu wa zamani , Edward Lowassa, ameendelea kuwa mstari wa mbele katika harakati zake za kuchangisha fedha baada ya kuchangisha zaidi ya Sh. Milioni 421.8 kwa ajili ya kuboresha Mfuko wa Elimu Kata ya Kipawa katika Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam.

Katika harambee hiyo iliyofanyika Hoteli ya Kilimanjaro Kempiski Dar es Salaam, Lowassa ambaye ni mbunge wa Monduli alichangia Sh.milioni 10.

Katika harambee hiyo miongoni mwa makampuni yaliyochangia kiasi kikubwa ni Lion Club Sh.milioni 70, Home Shipping Center Sh.milioni 22, African Barrick Gold Dola 10,000, Songas Dola 10,000, Maersk Sea Line ilichangia Sh.Miliono 90, na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja alichangia milioni Sh.10.

Wengine waliochangia ni madiwani, viongozi wa Chama Cha Mapinduzi, Chadema, taasisi za watu binafsi na mtu mmoja mmoja ambapo Radio Clauds walitoa muda wa hewani wa kutangaza mpango huo wenye thamani ya sh. milioni 12.

Akizungumza kabla ya kuendesha harambee ya kuchangisha, amewataka Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuendelea kuwahamasisha wananchi kuwekeza katika kuchangia sekta ya elimu.

Lowassa amempongeza Diwani wa Kata ya Kipawa, Bonnah Kaluwa, kwa jitihada zake alizozionyesha za kuchangia elimu na kuwataka madiwani wengine kuiga mfano huo.

Diwani wa Kata ya Kipawa, Bonnah Kaluwa, alisema shule saba za Msingi na Sekondari zilizopo kata hiyo zinakabiliwa na changamotonyingi zikiwemo za upungufu wa vyumba vya madarasa hali inayosababisha wanafunzi kati ya 140 hadi 160 kusomea katika darasa moja huku wakiwa wamekaa chini.

Kaluwa amesema jitihada nyingine zilizofanywa katika kutafuta pesa kwa ajili ya kuziboresha shule hizo ambapo Machi 17 mwaka huu kuliitishwa matembezi ya hisani yaliyoongozwa na mke wa Rais Mama Salma Kikwete.

Aliongeza kuwa katika hafla hiyo kiasi cha shilingi milioni 15 kilichangwa na wadau mbalimbali ambapo kati ya hizo Sh.Milioni 3 zilitolewa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete na Clouds Media Group ambao walitoa shilingi milioni moja na wanafunzi kadhaa wa shule za msingi na sekondari.

Mbunge wa Jimbo la Segerea Dk.Makongoro Mahanga alisema katika jimbo hilo shule nyingi zinakabiliwa na changamoto nyingi hivyo alitoa mwito kwa wananchi na madiwani wa eneo hilo kuunga mkono jitihada za kuchangia elimu ili kuwaondolea wanafunzi adha wanayopata ya kukosa mazingira bora ya kupata elimu.

No comments:

Post a Comment