Monday, June 4, 2012

TANZANIA POLITICAL NEWS: MBOWE KUJIUZULU CCM IKISALIMIKA 2015

MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amesema moto uliowashwa na chama hicho katika Operesheni Sangara utaendelea nchi nzima, lengo likiwa ni kuiondoa CCM madarakani na iwapo itasalimika mwaka 2015, atajiuzulu siasa.

Mbowe alitoa kauli hiyo juzi alipohutubia mamia ya wakazi wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara wakati chama hicho kilipofanya mkutano mkubwa kwenye uwanja wa mpira wilayani humo.
Alisema CCM kimepoteza mwelekeo wa kuongoza taifa na ndiyo sababu maisha ya Watanzania yamezidi kuwa mgumu kadri miaka inavyozidi kusonga mbele.

Mbowe alikishambulia CCM akidai kimepoteza mwelekeo uliowekwa na waasisi wake, chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere wa kuzingatia usawa, udugu huku kikijikita katika msingi wa kutetea wakulima wanyonge na wafanyakazi lakini sasa kimewagawa wananchi katika matabaka ya walio nacho na wasio nacho.

Katika mkutano huo uliokutanisha viongozi wote wa kitaifa wa chama hicho, Mbowe alisema kwa sasa CCM kimevuruga hata mitalaa ya elimu huku akituhumu watunga sera kuwa wanafanya hivyo makusudi kwa kuwa watoto wao hawasomi katika shule hizo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa alieleza kusikitishwa kwake na umaskini unaoukabili Mkoa wa Mtwara licha ya kuwapo rasilimali nyingi zinazouzunguka ikiwamo gesi na korosho.

Amesema kumekuwa na ufisadi mkubwa unaofanywa katika ununuzi wa korosho na licha ya wananchi kukatwa Sh30 katika kila kilo wanayouza, bado mikoa hiyo ya kusini inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, huduma muhimu za kijamii kama zahanati na shule.

No comments:

Post a Comment