Friday, June 8, 2012

SAFA YATAJA WATANO KUGOMBEA NAFASI YA MOSIMANE.

Pitso Mosimane.
SHIRIKISHO la Soka la Afrika Kusini-SAFA limetangaza majina ya makocha watano ambao watawania nafasi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo maarufu kama Bafana Bafana baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Pitso Mosimane kutimuliwa wiki iliyopita. Kamati ya Utendaji ya SAFA chini ya mwenyekiti wake Fanyana Sibanyoni ilikutana jana ambayo pamoja na mambo mengine pia walijadili suala la mchakato wa kumtafuta kocha mpya wa Bafana Bafana. Katika mchakato huo kamati imetoa kipaumbele kwa kocha mzawa ambaye atakuwa ametimiza vigezo wanavyovihitaji kuwa na nafasi kubwa ya kupewa kibarua hicho. Majina yaliyotangazwa na kamati hiyo ni pmaoja na Steve Komphela ambaye ndiye msimamizi wa Bafana Bafana baada ya Mosimane kuondoka, Gordon Igesund ambaye ni kocha wa Moroka Swallows, Gavin Hunt kocha wa Supersport United, Aliyekuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 na Bafana Bafana Ephraim Mashaba na Neil Tovey anayefundisha klabu ya Thanda Royal Zulu. Makocha watafanyiwa usaili Jumatatu Juni 18 ambapo Juni 30 mwaka huu kamati hiyo inatarajia kutangaza kocha mpya atakayeifundisha Bafana Bafana.

No comments:

Post a Comment