Wednesday, June 6, 2012

MBEYA UPDATE: TGNP YAIBUKA MASUALA TATA


MTANDAO wa jinsia Tanzania (TGNP) umeanza kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali vya habari nchini kama njia ya kusaidia kuibua mambo mbali mbali yaliyoibuka katika wilaya ya Mbeya vijijini .


Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo jana jijini Mbeya Kenny Ngomuwo alisema kuwa Kuanzia tarehe 21 hadi 31 Mei 2012, kikundi cha waraghbishi kutoka TGNP wamefanya mchakato shirikishi wa uraghbishi katika vijiji vya Nsongwi Juu, Ifiga, Iwalanje, Nsongwi Mantanji na Ntangano Ijombe,Kata ya Ijombe, Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani Mbeya.

Alisema kuwa wakazi wa Kata ya Ijombe wameelezea kero mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao wanayolima, ambapo madalali hununua mazao kwa bei ndogo na kwenda kuuza kwa wafanyabiashara wakubwa bila wao kupata faida. Sambamba na hilo, ushuru pia ni kero kubwa.

Pia alisema wamekuwa wakilalamikia ushuru wa aina mbili ukiwemo ushuru wa mazao shambani na ushuru wa mazao yakifika sokoni, ambao wanalipa bila stakabadhi kutolewa. Kwa ushuru wa shambani kila gunia ni shilingi 1000/- na ushuru wa mazao sokoni ni shilingi 200/- kwa mchuuzi. Wakati huo huo, wakazi wa Ijombe wamedai katika Kata yao hakuna utawala bora kwani baadhi ya viongozi hawaweki wazi taarifa za mapato na matumizi na huu ni uvunjaji wa sheria. 

Alisema kuwa ushuru huo umekuwa ni mzigo mkubwa kwa wanawake wa Ijombe na wameuomba uongozi husika hasa katika ngazi za vitongoji, vijiji na Kata waweze kufuatia kero hizi na kuweka sheria zitakazowabana wanaume kutokana na vitendo vyao. 

Pia wakazi wa Ijombe wameomba uongozi kufuatilia na kudhibiti muda wa kuuza pombe. Wanapendekeza vilabu vifunguliwe kwa muda maalum uliopangwa. Kisheria vilabu vinapaswa kufunguliwa saa kumi jioni na kufungwa saa tatu usiku, na sio kufunguliwa saa moja asubuhi kama ilivyo kwa sasa.

Kero nyingine waliyotoa ni mimba za utotoni kutokana na ukosefu wa mabweni kwa wasichana wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Iwalanje.

Aidha alisema kuwa Shule ya Iwalanje imekuwa mbali sana na makazi ya walio wengi. Wanafunzi wanatembea umbali wa kati ya kilometa 4 hadi 8 kutoka vijiji vinavyotumia shule hiyo.
Tatizo hili la umbali limepelekea baadhi ya wanafunzi kupanga vyumba vinavyojulikana kwa jina maalum la ‘GHETO’.

Wakazi wa Kata hiyo wamedai kuwa kutokana na kuishi kwenye magheto kwa muda mrefu kumepelekea wasichana wengi kutokufanya vizuri katika masomo yao.

Wasichana walio wengi, wamegeuka kuwa wapishi na wanasaka maji, kuni kwa ajili ya kujipikia chakula.

Hivyo alisema kuwa wanahabari hao zaidi ya 15 watakwenda kufanya utafiti wa kina katika maeneo hayo na kuibua matatizo mengi zaidi ya hayo.

Imeandikwa na Francis Godwin aliyekuwepo Mkoani Mbeya kwa ajili ya utafiti

No comments:

Post a Comment