Tuesday, June 5, 2012

GLOBAL NEWS: WANANCHI WA MISRI WANATAKA SERIKALI YA KIISLAMU


Msemaji wa chama cha Uhuru na Uadilifu cha Misri amesema kuwa, wananchi walio wengi wa nchi hiyo wanataka serikali ya wananchi chini ya misingi ya Uislamu.
 
Waleed el Haddad ameiambia televisheni ya Press TV kuwa, wananchi wa Misri ambao wana ustaarabu mkongwe wa dini tukufu ya Kiislamu, wanapenda kuona mafundisho ya Uislamu - ya kutotenganishwa dini na siasa - yanatekelezwa nchini humo, na wanapinga utawala wa kisekula, unaopinga dini.

Msemaji huyo ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kisiasa ameongeza kuwa, kamwe wananchi wa Misri hawatokubali kurejea utawala wa dikteta Hosni Mubarak kwa mlango wa nyuma na kwamba watasimama kidete kukabiliana na njama zote za kuurejesha madarakani utawala huo. Kabla ya hapo pia, Ali Khaffaji, mmoja wa viongozi waandamizi wa chama cha Uhuru na Uadilifu cha Misri ameyataja matamshi ya Ahmad Shafiq, Waziri Mkuu wa mwisho wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak kuwa ni kichekesho na kusisitiza kuwa, vyama vya upinzani nchini Misri vitaendelea na maandamano yao hadi vitakapofanikisha malengo ya mapinduzi ya wananchi wa nchi hiyo ambayo ni pamoja na usawa, uhuru na uadilifu.
Itakumbukwa kuwa, Ahmad Shafiq ametoa tuhuma kali dhidi ya chama cha Uhuru na Uadilifu na pia amewataka wananchi wa Misri wakubaliane na hukumu ya mahakama ya nchi hiyo iliyowaondolea tuhuma wana wawili wa dikteta Hosni Mubarak na kumhukumu adhabu nyepesi firauni huyo wa Misri.
 

Ahmad Shafiq, Waziri Mkuu wa mwisho wa utawala wa dikteta Hosni Mubarak, na Mohammed Morsi wa chama cha Uhuru na Uadilifu ambalo ni tawi la kisiasa la kundi la Ikhwanul Muslimin nchini Misri wanatarajiwa kuchuana katika duru ya pili ya uchaguzi wa nchi hiyo unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 na 17 mwezi huu wa Juni.

No comments:

Post a Comment