Monday, June 11, 2012

EURO 2012: URUSI YAWAONYA MASHABIKI WAKE.

SHIRIKISHO la Soka la Urusi limewaonya mashabiki wake jana kuwa vitendo vya kihuni wanavyofanya vinaweza kusababisha timu ya taifa ya nchi hiyo kupokwa pointi katika michuano ya Ulaya baada ya Shirikisho la Soka la Ulaya-UEFA kuanza uchunguzi kutokana na taarifa za vurugu zilizotokea katika mchezo wao wa kwanza dhidi ya Jamhuri ya Czech. Picha za video zilionyesha mashabiki wa Urusi wakipambana na polisi waliokuwa wakilinda usalama uwanjani jijini Wroclaw na UEFA wamesema kuwa pia watachunguza matukio ya ubaguzi yanayodaiwa kutokea kwa mchezaji wa Czech ambapo Urusi ilishinda kwa mabao 4-1. Katika taarifa iliyotolewa na shirikisho hilo katika mtandao wake iliwaonya mashabiki wa timu hiyo waliofunga safari ya kuja kuishangilia timu hiyo kujiheshimu wenyewe, kuiheshimu timu pamoja na nchi yao na kusisitiza kuwa wasipofanya hivyo wanaweza kusababisha timu yao kutolewa katika michuano hiyo. Taarifa hiyo pia ilisema mashabiki hao wanaruhusiwa kuandika mabango ambayo yatakuwa yakiipa moyo timu yao na sio mabango yahusuyo mambo ya kisiasa kwani hayatapewa nafasi wakati timu hiyo ikiwa inacheza. Kiongozi wa shirikisho la soka la Urusi na kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo jana walitembelea makaburi ambayo rais wa Poland na watu wengine 95 walizikwa kufuatia ajali ya ndege iliyotokea mwaka 2010 nchini Urusi.

No comments:

Post a Comment